Liverpool, England
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ametangaza kuachana na timu hiyo mara baada ya msimu huu kwa kile alichosema kwamba ‘amechoka’.
Klopp alijiunga na Liverpool Oktoba mwaka jana akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani na mkataba wake wa sasa na timu hiyo unafikia mwisho mwaka 2026 lakini ameamua kuachana na timu hiyo kabla ya mkataba kufikia mwisho.
Akiwa na Liverpool, Klopp ameiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019 na taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2019-20 ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kubeba taji hilo baada ya miaka 30.
Klopp mwenye umri wa miaka 56 na ambaye timu yake kwa sasa inashika usukani EPL, alisema alishauarifu uongozi wa klabu hiyo tangu Novemba mwaka jana na anaelewa kwamba uamuzi huo utawashtua wengi.
“Naelewa ni uamuzi unaoshitua watu wengi kwa wakati huu, pale unaposikia kwa mara ya kwanza lakini naweza kuelewa hilo au walau kujaribu kutoa ufafanuzi,” alisema Klopp.
“Napenda karibu kila kitu katika klabu hii, napenda kila kitu kuhusu jiji hili, napenda kila kitu kwa mashabiki wetu, naipenda timu, nawapenda maofisa, napenda kila kitu lakini bado nimeamua kuchukua uamuzi, hiyo ni kuwaonesha kwamba ni mimi mwenyewe ndiye niliyelazimika kuchukua uamuzi huu,” alisema Klopp.
“Hivyo ndivyo nilivyoamua, nawezaje kulisema hilo la kuishiwa nguvu, sina tatizo nilifahamu tangu awali kwamba kuna wakati nitalazimika kutangaza, lakini kwa sasa niko sawa,” alisema.
“Baada ya kuwa pamoja kwa miaka mingi na baada ya kushirikiana kwa muda mrefu na yale yote tuliyopitia pamoja, nimejenga heshima kwenu, mapenzi kwenu yamekuwa, huo ndio ukweli,” alisema Klopp.
Liverpool chini ya Klopp imefanikiwa kubeba karibu mataji yote makubwa kuanzia Ligi ya Mabingwa Ulaya, EPL, Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Fifa.