Madrid, Hispania
Jaji mmoja wa Mahakama Kuu ya Hispania ametaka aliyekuwa kiongozi wa soka nchini humo, Luis Rubiales ashitakiwe kwa kitendo cha kumpiga busu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Hispania, Jenni Hermoso.
Rubiales alimshika shingoni Jenni na kumpiga busu la mdomoni wakati wa utoaji tuzo baada ya Hispania kuibwaga England na kubeba Kombe la Dunia la Wanawake Agosti mwaka jana katika mechi ya fainali iliyopigwa mjini Sydney, Australia.
Kwa mujibu wa jaji huyo, upo ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi hiyo huku akitaja kitendo hicho kuwa hakikuwa na maridhiano baina ya Jenni na Rubiales.
Awali waendesha mashitaka walimshitaki Rubiales kwa kosa la udhalilishaji kijinsia na ubabe ambapo adhabu yake inaweza kuwa ni faini au kifungo cha jela miaka minne.
Tukio hilo pia limewaingiza matatizoni vingozi wengine watatu wa timu ya soka ya wanawake ya Hispania kuanzia aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Jorge Vilda, meneja masoko, Ruben Rivera na mkurugenzi wa michezo wa timu ya wanaume ya Hispania, Albert Luque.

Watatu hao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa kumshawishi Jenni kuueleza umma kuwa busu alilopigwa lilitokana na ridhaa yake na kwa mujibu wa jaji huyo, watu hao watatu nao wanapaswa kushitakiwa.
Rubiales aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Hispania awali alisimamishwa na Fifa kwa siku 90 licha ya kukana kufanya kosa lolote akidai Jenni aliridhia kupigwa busu hilo, baadaye alilazmika kujiuzulu uongozi baada ya kusakamwa kila kona.
Jenni ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji nyota wa timu ya Hispania, alinukuliwa akisema kwamba kitendo alichofanyiwa na Rubiales hakikubaliki na kuahidi kuitafuta haki.