Abidjan, Ivory Coast
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeshindwa kufuzu hatua ya mtoano kwenye fainali za Afcon baada ya kukubali sare ya 0-0 mbele ya DR Congo na hivyo kuaga rasmi fainali hizo kwa kuishia hatua ya makundi.
Stars katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano hii usiku ilihitaji ushindi wowote ili kufikisha pointi nne ambazo zingeifanya ifuzu hatua ya mtoano lakini sare imeifanya imalize ikiwa mkiani katika Kundi F.
Tofauti na matarajio ya wengi, Stars iliuanza mchezo huo kwa kuonesha uhai tangu mwanzo na kutoa dalili za kupata bao baada ya nahodha wake Mbwana Samatta kufika langoni mwa DR Congo katika dakika tatu za mwanzo.
Timu hiyo iliendelea kucheza kwa kujihami huku ikilisogelea lango la wapinzani wao ambao walijibu mapigo dakika ya 11 na kumlazimisha Himid Mao kucheza rafu na mwamuzi kuipa DR Congo mpira wa adhabu ambao ulipigwa na Gael Kakuta lakini haukuwa na madhara.
Dakika ya 29, Kakuta tena alimuunganishia pasi nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele ambaye alipita katikati ya mabeki wa Stars, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca lakini shuti alilopiga liliokolewa na kipa wa Stars, Aishi Manula.
Stars nao walikuja juu dakika ya 48 baada ya Novatus Dismas, Samatta na Lusajo Mwaikenda kugongeana pasi wakiwa karibu na lango la DR Congo lakini mpira wa kichwa uliopigwa na Novatus ulikuwa mwepesi mno kwa kipa wa DR Congo, Mpasi.
Katika kujiimarisha DR Congo iliwatoa Silas Katompa na nafasi yake kuingia Meshack Eliya na baadaye Mayele aliyekuwa na wakati mgumu kuipenya ngome ya Stars alitoka na kuingia Bikabu.
Kwa upande wa Stars Himid Mao alitoka na nafasi yake kuingia Muzamir Yassin,
Mabadiliko hayo yalionekana kuipa uhai DR Congo na kuongeza nguvu ya kulisakama lango la Stars na katika dakika ya 77 kama si umahiri wa Manula, DR Congo wangeweza kupata bao.
Manula ambaye alitoka katika eneo lake ili kuuwahi mpira lakini aliukosa na kulazimika kurudi nyuma kwa kasi, kabla hajafika katika eneo lake, Yoane Wissa aliupiga mpira wa juu na Manula kulazimika kuruka huku akirudi nyuma, akafanikiwa kuutoa mpira huo na kuwa kona.
Stars iliendelea kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Feisal Salum ‘Fei Toto na kumuingiza Kibu Denis kabla ya kuwatoa Simon Msuva na Samatta na nafasi zao kuchukuliwa na Charles Mmombwa na Moses Abraham.
Mabadiliko hayo hata hivyo hayakuwa na tija kwa Stars kwani hadi mwisho wa mchezo matokeo yalikuwa sare ya 0-0 na kuifanya Stars iage fainali hizo mapema katika hatua ya makundi.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Morocco iliichapa Zambia bao 1-0 na hivyo kumaliza mechi zake za makundi ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na DR Congo yenye pointi nne ambazo ndizo zilizofuzu katika kundi hilo, Zambia ya tatu ikiwa na pointi mbili kama Stars iliyoishia mkiani.
Hii ni mara ya tatu katika historia ya Stars kushiriki Afcon na kuishia hatua hiyo, ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1980 na baadaye mwaka 2019.
Kimataifa Stars yaaga Afcon mapema
Stars yaaga Afcon mapema
Read also