Na mwandishi wetu
Kipa wa Tabora United, John Noble amesema anatamani siku moja kujiunga na timu kubwa za Dar es Salaam, hasa Simba na Yanga lakini pindi atakapomaliza mkataba na timu yake anayoitumikia hivi sasa.
Akizungumza na GreenSports, kipa huyo raia wa Nigeria alisema kinachomvutia kwa timu hizo ni namna mashabiki wanavyozipenda timu zao lakini pia upinzani wa kusaka mafanikio ya ndani ya uwanja.
“Nimekuwa hapa kwa miezi mitano, ukweli nimevutiwa sana na upinzani wa Simba na Yanga katika mambo mengi, kwanza ushindani waliokuwa nao katika kusaka mafanikio lakini namna mashabiki wanavyozipenda na kuzituatilia timu zao,” alisema Noble.
Kipa huyo aliyewahi kupita Enyimba International ya kwao Nigeria, alisema mbali na hivyo lakini ushiriki wa michuano ya kimataifa pamoja na maslahi mazuri ni miongoni mwa vitu vinavyomshawishi kupenda kuzitumikia timu hizo kwa siku zijazo.
Klabu za Simba na Azam FC, ziliwahi kuripotiwa kuhitaji huduma ya kipa huyo mwanzoni mwa msimu kabla ya uongozi wa Tabora United kuweka ngumu kwa kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja.
Soka Noble azitamani Simba, Yanga
Noble azitamani Simba, Yanga
Read also