Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameeleza kuridhishwa na viwango vinavyooneshwa na wachezaji wake wanaoshiriki michuano ya Afcon wakiwa na timu zao za taifa nchini Ivory Coast.
Katika michuano hiyo, Yanga imetoa wachezaji saba ambao wanatoka kwenye mataifa manne tofauti; Tanzania, Zambia, Burkina Faso na Mali.
Wachezaji hao ni Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Mudathir Yahya na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Tanzania. Wengine ni Djigui Diarra (Mali), Kennedy Musonda (Zambia) na Stephane Aziz Ki (Burkina Faso).
“Kikosi changu kimetoa wachezaji saba, wengi wanaanza kwenye timu zao na nimekuwa nawafuatilia kwa makini, ukweli naridhishwa na viwango vyao na hata ambao hawapati nafasi ya kuanza si kwamba hawana uwezo bali ni mapendekezo ya kocha,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema uwajibikaji wao wakiwa na timu zao za taifa unampa kazi nyepesi kuwaunganisha na wenzao ambao hawakuitwa kwenye timu za taifa kwa ajili ya michuano hiyo ya Afrika.
Alisema mpango wake ni kuwa na kikosi imara kitakachopambana na kufanya vizuri kwenye mashindano yote yanayowakabili ikiwemo mechi mbili zilizosalia za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa sasa kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi kambini kwao Avic Town, Kigamboni mjini Dar es Salaam kikijiandaa na mechi za Ligi Kuu NBC, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa wakipigania kufuzu hatua ya robo fainali.