Conakry, Guinea
Shirikisho la Soka Guinea (Feguifoot) limetaka kuwepo utulivu baada ya kutokea vifo vya mashabiki sita wa soka nchini humo waliokuwa wakishangilia ushindi wa kwanza wa timu yao kwenye fainali za Afcon zinazoendelea Ivory Coast.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Ijumaa iliyopita, Guinea iliichapa Gambia bao 1-0 hali iliyoibua mlipuko wa furaha miongoni mwa mashabiki ambao waliingia mitaani wakishangilia ushindi huo.
Kwa mujibu wa Feguifoot, vifo vya mashabiki hao vilitokea katika mji wa Conakry baada ya mashabiki baadhi yao wakiwa kwenye magari na wengine pikipiki kuingia mitaani na kushangilia ushindi huo.
Vyanzo vingi vya habari hata hivyo havijaeleza kwa undani kuhusu vifo hivyo vimesababishwa na nini hasa, umri wa waliofariki, jinsia zao pamoja na idadi ya majeruhi kama wapo.
Tukio la vifo hivyo limetokea wakati baadhi ya mashabiki wa Guinea wapo nchini Ivory Coast kwa ajili ya kuishangilia timu yao ya taifa wakati wale walio nyumbani wengi wao wanafuatilia mechi za timu hiyo kupitia televisheni.
Bao pekee lililoipa Guinea ushindi katika mechi hiyo ya Kundi C lilifungwa na Aguibou Camara katika dakika za majeruhi na kuipa timu hiyo ushindi ambao pia umeibua matumaini ya timu hiyo kusonga mbele baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Cameroon.
Guinea, ni moja ya nchi ambazo wananchi wake wana mapenzi makubwa ya soka na haikushangaza kwa wananchi kuingia barabarani kushangilia ushindi dhidi ya Gambia mara tu baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo.
Kimataifa Mashabiki sita wafariki Guinea
Mashabiki sita wafariki Guinea
Read also