Na mwandishi wetu
Nyota wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamesema malengo yao ni kuhakikisha wanavuna pointi sita zilizobaki kwenye hatua ya makundi ya Afcon ili wajiweke kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata.
Stars ilianza ibaya michuano hiyo kwa kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Morocco ambao ndio vinara wa Kundi F wakati kichapo hicho kikiwashusha Tanzania mkiani mwa msimamo.
Nahodha msaidizi wa Stars, Himid Mao (pichani juu) alisema wanamshukuru Mungu wako sawa baada ya mchezo, wanaendelea vizuri, wamesahau matokeo ya mchezo uliopita na kwa maandalizi wanayofanya anaamini mechi ijayo watapata ushindi.
“Kwa sababu tayari tumepoteza pointi tatu kati ya tisa zilizobaki za kupigania ni sita, hivyo inabidi tupambane kadri inavyotakiwa ili tupate matokeo katika mchezo ujao, kama tukipata matokeo kwenye mechi na Zambia, naamini itatupa picha nini kilichopo mbele yetu,” alisema Mao.
Mshamabuliaji Simon Msuva: “Tunawaomba Watanzania wazidi kutuombea kwa uwezo wa Mungu tutafanya vizuri hatutawaangusha, tunajua mechi ya kwanza wameumia kwa matokeo yaliyotokea lakini mechi inayofuata naamini tutafanya vizuri,” alisema Msuva.
Naye beki Abdi Banda hakuwa mbali na maoni ya Mao na Msuva, akisema: “Nafasi ipo bado kubwa kwa sababu kupoteza mchezo wa kwanza haimaanishi kuwa umetoka kwenye mbio za hatua inayofuata, kuna mechi mbili kubwa tunacheza, tunarudi uwanjani kupambana ili kupata matokeo hakuna kitu kingine,” alisema Banda.
DR Congo na Zambia wanaoshika nafasi ya pili na tatu, katika mechi yao ya kwanza walitoka sare ya bao 1-1.