Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa zamani wa Simba, Patrick Phiri (pichani) ameisifia timu hiyo kwa kumnasa kinara wa mabao wa Ligi Kuu Zambia, Freddy Kouablan kutoka Green Eagles akiamini ni usajili wa nguvu utakaowabeba Wekundu hao.
Freddy raia wa Ivory Coast ametambulishwa Simba leo Ijumaa kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuweka rekodi nzuri Ligi Kuu Zambia akiwa ameifungia mabao 14 na kutoa pasi nne za mabao katika mechi 18.
Phiri ambaye amewahi kuiongoza Simba mara tatu msimu wa 2003-05, 2008-11 na 2014-15, alisema klabu hiyo imelamba dume kwa kumpata straika sahihi ambaye atawavusha kwenye malengo yao.
“Ni mshambuliaji mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kufunga akiwa Ligi Kuu Zambia, ameonyesha ni mchezaji wa daraja la juu, naamini atawapa vitu vingi sana.
“Kama ataendelea na kasi aliyoianza huku Zambia naamini ataenda kuziba mapengo yaliyoachwa na washambuliaji waliopita kwani shabaha yake ni nzuri mbele ya lango lakini pia anaweza kuwatengenezea wengine nafasi,” alisema Phiri.

Alisema faida nyingine kwa Simba kwa mchezaji huyo kama akiwa fiti, anaweza kutumika kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani timu yake haikuwa sehemu ya wawakilishi wa Zambia kwenye mashindano hayo ya CAF.