Barcelona, Hispania
Kocha wa Barcelona, Xavi amesema kwamba atabeba mabegi yake na kuondoka katika klabu hiyo kama wachezaji watapoteza imani kwake.
Barca Jumapili ililala kwa mabao 4-1 mbele ya mahasimu wao Real Madrid katika mechi ya fainali ya Super Cup Hispania wakati kwenye Ligi Kuu Hispania au La Liga timu hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa nyuma ya pointi nane mbele ya vinara, Girona.
“Naipenda hii klabu, nipo hapa kwa ajili ya kuleta mambo makubwa, kama sitofanya hayo nitarudi nyumbani,” alisema Xavi kiungo wa zamani wa timu hiyo ambaye alikabidhiwa jukumu la kuwa kocha Novemba 2021.
“Ningeshindwa kubeba taji la La Liga mwaka jana nisingekuwa hapa, itakapofika siku wachezaji wakawa hawanifuati mimi hapo nitabeba mabegi yangu na kuondoka, kama mtu ataniambia kwamba kuna tatizo hapa nitaondoka,” alisema Xavi.
Xavi ambaye ameshinda tuzo 25 enzi zake akiichezea klabu hiyo kwa mafanikio kabla ya kugeukia kazi ya ukocha ambapo alianzia Qatar alipokuwa akiinoa klabu ya Al Sadd.
Leo Alhamisi Barca itaumana na Unionistas katika kuwania taji la Hispania na katika Ligi ya Mabingwa timu hiyo imo katika 16 bora ikisubiri kuumana na Napoli.
“Wamiliki waliponiajiri kutoka Qatar waliniambia kilikuwa kipindi cha hovyo mno katika historia ya klabu na hapa tupo katika mchakato wa kubadili mambo, nimetulia, nina mataji matatu ya kuyashinda, tuko karibu mno na mafanikio kuliko kushindwa,” alisema Xavi.