Roma, Italia.
Klabu ya AS Roma imetangaza kuachana na kocha Jose Mourinho na tayari kiungo wa zamani wa timu hiyo, Daniele De Rossi amekabidhiwa majukumu ya kuwa kocha wa muda hadi mwisho wa msimu huu.
Mkataba wa Mourinho na klabu hiyo ulikuwa unafikia mwisho baada ya msimu huu lakini kipigo cha mabao 3-1 ambacho Roma imekutana nacho Jumapili iliyopita huenda kimechangia kumuondoa kocha huyo katika timu ambayo pia inashika nafasi ya tisa katika Serie A.
Uamuzi wa kuachana na Mourinho ulitangazwa jana Jumanne kwa kilichoelezwa kwamba kocha huyo na wamiliki wa klabu wameamua kuachana.
Mourinho alianza kuinoa Roma Mei 2021 na kuiwezesha kubeba taji la Europa Conference Ligi mwaka 2022 na kufikia hatua ya fainali ya Europa Ligi mwaka uliofuata.
“Tunapenda kumshukuru Jose kwa niaba yetu hapa Roma kwa namna alivyoonesha mapenzi na juhudi tangu kuwasili katika klabu hii, ilieleza taarifa ya wamiliki wa klabu hiyo, Dan na Ryan Friedkin.
“Wakati wote tutaendelea kuwa na kumbukumbu za wakati wake akiwa Roma lakini tunaamini mabadiliko ya haraka ni jambo zuri kwa manufaa ya klabu, tunamtakia Jose na wasaidizi wake kila la heri katika mambo yao yajayo,” ilieleza taarifa hiyo.
Mourinho amekuwa akihisishwa na mipango ya kwenda Saudi Arabia na amewahi kunukuliwa akisema kwamba kuna siku atafanya kazi Saudi Arabia.
Pia amewahi kuhusishwa na mipango ya kukinoa kikosi cha Brazil lakini alikanusha habari hizo kwa kile alichodai kwamba hakuwahi kuzungumza yeye au wakala wake na kiongozi yeyote wa soka nchini Brazil.