London, Uingereza
Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi ameshinda tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa wakati kocha wa Man City Pep Guardiola akishinda tuzo ya kocha bora.
Messi ambaye pia anaichezea klabu ya Inter Miami ya Marekani, amewabwaga washambuliaji wawili mahiri, Erling Haaland wa Man City na Kylian Mbappe.
Katika tuzo hizo, kipa wa Man City Ederson yeye ametwaa tuzo ya kipa bora akimbwaga kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois na Yassine Bounou wa Al Hilal.
Mafanikio ya kipa wa Man City kwa kiasi kikubwa yamebebwa na rekodi nzuri ya klabu hiyo kwenye msimu wa 2022-23 baada ya kubeba mataji matatu (treble) ya Ligi ya Mabingwa, FA pamoja na Ligi Kuu England.
Kwa Messi, nyota wa zamani wa Barcelona na PSG, hii inakuwa mara ya tatu kubeba tuzo hiyo ya Fifa tangu utaratibu wa tuzo hizo uanzishwe mwaka 2016, awali alibeba mwaka 2019 na 2022.
Wachezaji wafuatao pia wameteuliwa katika timu bora ya mwaka kwa upande wa wanaume; Thibaut Courtois (Real Madrid), John Stones, Kyle Walker, Ruben Dias na Bernardo Silva (Man City), Jude Bellingham (Real Madrid), Kevin de Bruyne na Erling Haaland (Man City), Kylian Mbappe (PSG), Lionel Messi (Inter Miami) na Vinicius Jr (Real Madrid).
Tuzo za mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa huwa zinaangalia kalenda ya mwaka, ni tofauti na tuzo maarufu za Ballon d’Or ambazo zinaangalia mafanikio ya mchezaji husika katika msimu mmoja.
Kimataifa Messi mchezaji bora wa Fifa
Messi mchezaji bora wa Fifa
Read also