Abidjan, Ivory Coast
Bao la penalti la dakika za lala salama la nahodha wa Misri, Mohamed Salah limeiwezesha timu hiyo kutoka sare ya mabao 2-2 na Msumbiji katika mechi ya Kundi B ya fainali za Afcon zinazoendela nchini Ivory Coast.
Misri waliianza mechi hiyo vizuri kwa kuandika bao la kwanza mapema sekunde ya 88 lililofungwa na Mostafa Mohamed lakini matarajio ya timu hiyo kutoka na ushindi yalifutika kipindi cha pili kwa mabao ya Witi na Clesio.
Mabao hayo yalitoa kila dalili za jahazi la Misri kuzama kabla mwamuzi hajaamuru ipigwe penalti baada ya Domingos Macandza kumshika mchezaji mmoja wa Misri katika eneo la penalti na Salah hakufanya ajizi kuujaza mpira wavuni.
Uamuzi wa kuipa Misri penalti ulifikiwa baada ya mwamuzi Dahane Beida kutumia VAR kufanya mapitio na ndipo alipojiridhisha kwamba Misri ilikuwa sahihi kupewa penalti.
Salah amewahi kunukuliwa akisema kwamba atapenda kushinda taji la Afcon mara ya kwanza na timu ya Misri baada ya kufikia hatua ya fainali mara mbili ingawa bado timu hiyo ina kazi ngumu, Alhamisi itakuwa na mechi ya pili dhidi ya Ghana.
Matokeo ya mechi za Afcon jana Jumapili
Nigeria 1-1 Equatorial Guinea
Misri 2-2 Msumbiji
Ghana 1-2 Cape Verde
Kimataifa Salah aokoa jahazi Misri
Salah aokoa jahazi Misri
Read also