Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ameuagiza uongozi wa timu hiyo kumtafutia mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao na kufanikisha lengo la kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu.
Inadaiwa kuwa kocha huyo hajaridhishwa na viwango vya washambuliaji Moses Phiri na Jean Baleke ndio sababu ya kuuagiza uongozi wa timu hiyo kuharakisha mchakato wa kumpata mshambuliaji mpya.
Kocha huyo alisema ana orodha ya washambuliaji wengi wenye uwezo wa kuisaidia timu hiyo kufika hatua hiyo kitu cha msingi ni kutoa ruhusa aanze mchakato kabla dirisha la usajili halijafungwa.
“Washambuliaji tulionao ni wazuri kwenye mashindano ya ndani lakini kutokana na malengo tuliyonayo kwenye Ligi ya Mabingwa, tunahitaji mtu ‘katili’ kutufikisha nusu fainali, tazama tulivyopata tabu kwenye Kombe la Mapinduzi,” alisema Benchikha.
Benchikha alisema tangu atue Simba, anafurahishwa namna uongozi unavyomsikiliza na kuyafanyia kazi mapendekezo yake, hivyo hata suala la mshambuliaji anaamini watalipa uzito sababu lengo lake ni kuona linakamilika kwa wakati.
Alisema kwa timu yenye kutaka mafanikio hasa kubeba ubingwa wa Afrika, huwa haijifikirii kutoa kiasi kikubwa cha pesa kununua mchezaji mzuri na kwa Simba wanatakiwa kufanya hivyo ili kufikia walipo Wydad AC, Al Ahly na timu nyingine zenye mafanikio Afrika.
Simba ipo nafasi ya pili kwenye Kundi B Ligi ya Mabingwa, wakifunga mabao matatu jambo ambalo kocha huyo alisema halimpendezi ukizingatia kundi hilo timu zimeachana kwa idadi ndogo ya pointi hivyo mabao yanaweza kutoa maamuzi. .