Manchester, England
Winga wa Man United, Antony amekuwa na wakati mgumu kurudi kwenye ubora wake jambo ambalo kocha wake, Erik ten Hag anasema limesababishwa na matatizo ya nje ya uwanja yanayomuandama mchezaji huyo.
Septemba mwaka jana, Antony alilazimika kuwa nje ya klabu hiyo kwa kipindi cha wiki tatu baada ya kujikuta katika tuhuma za kumdhalilisha mwanamke.
Polisi nchini Brazil pamoja na Uingereza wanaendelea na uchunguzi wa sakata hilo na Ten Hag anasema mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil kwa msimu huu hajafunga hata bao moja au kutoa asisti jambo ambalo anaamini linachangiwa na matatizo yake ya nje ya uwanja.
“Naweza kulielezea hilo na nafikiri ni jambo rahisi, mambo yake ya nje ya uwanja yanamzuia kucheza,” alisema Ten Hag mbele ya waandishi wa habari leo Ijumaa.
“Mwaka wake wa kwanza ulikuwa sawa, kwenye maandalizi ya msimu alikuwa sawa, mechi nne za kwanza alikuwa vizuri lakini tangu awe nje ya timu na hadi anarudi hakuwa na kiwango ambacho ungekitarajia kutoka kwake na ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi,” alisema Ten Hag.
“Haya mambo yamemuathiri na hakika yamekuwa na matokeo mabaya kwake, ni lazima akabiliane nayo, ayamalize lakini pia ana wajibu wa kucheza vizuri,” alisema Ten Hag.
Katika hatua nyingine Ten Hag amemtakia heri winga wake wa zamani Jadon Sancho baada ya kuhamia kwa mkopo Borussia Dortmund ingawa hakutaka kusema kama mchezaji huyo ana nafasi katika klabu hiyo kwa siku zijazo.