Na Hassan Kingu
Fainali za soka za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2024 zinatarajia kuanza kuunguruma kesho Jumamosi nchini Ivory Coast ambapo mataifa 24 yanashiriki michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya timu za taifa Afrika.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa hayo na wanashiriki kwa mara ya tatu baada ya kuwemo mwaka 1980 nchini Nigeria, 2019 kule Misri na mwaka huu nchini Ivory Coast.
Achana na rekodi ya ushiriki wa Tanzania ambayo si nzuri sana kwa kuwa timu hiyo haijawahi kuvuka hata hatua ya makundi, lakini kikubwa tunaangazia wachezaji wakongwe au wenye uzoefu waliomo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki Afcon 2019 na msimu huu wamejumuishwa tena.
Nyota hao ambao wataungana na wachezaji wengine wanaoshiriki kwa mara ya kwanza kama Bakari Mwamnyeto, Kwesi Kawawa na wengine ni pamoja na kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya, Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Azam FC) na Simon Msuva (mchezaji huru).
Wengine ni Himid Mao (Ghazl El Mahalla ya Misri), Aishi Manula na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ (wote kutoka Simba) na nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta (PAOK FC ya Ugiriki).
Wachezaji hao saba ni miongoni mwa kikosi cha wachezaji 23 kilichoitwa na kocha mkuu wakati huo, Mnigeria, Emmanuel Amunike na kumaliza nafasi ya mwisho katika Kundi C lililokuwa na timu za Kenya, Algeria ambao ndio walikuwa mabingwa na Senegal waliomaliza nafasi ya pili.
MANULA
Kipa huyo mashuhuri alikuwa chaguo la kwanza kwenye Afcon 2019 na hiyo ilitokana na kiwango bora alichokionesha kwenye Ligi Kuu NBC lakini pia michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Msimu huu amejumuishwa tena kwenye kikosi hicho chini ya kocha Adel Amrouche akipambana na Kawawa anayecheza soka timu ya Karlslunds IF FK ya Ligi Kuu Sweden na Beno Kakolanya wa Singida Fountain Gate.
Mchango wa Manula kwa Stars msimu huu unatia mashaka ingawa bado haijajulikana kama Amrouche atamtumia kama kipa chaguo la kwanza au vipi.
Na mashaka hayo yanatokana na kipa huyo kukaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti aliyoyapata msimu uliopita akiwa na Simba na kusababisha kufanyiwa upasuaji.
Manula pia aliichezea Simba mara ya mwisho mchezo wa ushindani Novemba 5, mwaka jana ukiwa ni wa ligi kuu dhidi ya watani zao, Yanga ambapo aliruhusu kufungwa mabao matano, tangu hapo hajapata nafasi ya kucheza tena zaidi ya kufanya mazoezi.

Katika mechi zilizofuata za Simba, golini alisimama Ally Salim au Ayoub Lakred ambao wamekuwa wakionesha viwango vikubwa kama majuzi Salim alivyoisaidia Simba kutinga fainali ya Kombe la Mapinduzi akipangua penalti tatu za Singida Fountain Gate na Simba kushinda kwa matuta 3-2.
Hivyo, pamoja na uwepo wake lakini bado kuna mashaka juu ya mchango wake katika michuano hiyo iliyoteka hisia za Watanzania lukuki.
MUDATHIR
Mwaka 2019 alikuwa bado kijana mdogo wakati akiitumikia Azam FC, na Amunike alimchukua ili kwenda kupata uzoefu kwa ajili ya siku zijazo, alicheza mechi mbili kati ya tatu za hatua ya makundi na zote alitokea benchi.
Msimu huu amejumuishwa tena kwenye kikosi, akionekana yuko tayari kutokana umri alionao na pia uzoefu wa michuano ya klabu Afrika anayoshiriki na Yanga kwa sasa.
Mbali na kiungo huyo kuchukua tuzo ya bao bora la wiki kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuifikisha timu hiyo fainali lakini kiwango chake binafsi kimekuwa gumzo.
Kocha wa Yanga aliyepita, Nassredine Nabi alikuwa akimtumia kama silaha zake zenye thamani kubwa kama vile ambavyo kocha wao wa sasa, Miguel Gamondi anavyomtumia.
Kama Amrouche ataamua kuendelea kumtumia kwenye kikosi cha kwanza, yawezekana akawa msaada mkubwa katikati ya uwanja kwa Stars na kuwa kikwazo mno kwa wapinzani wao.
HIMID MAO
Himid anayemudu vizuri nafasi ya kiungo mkabaji, huyu ni kiungo mkabaji sifa yake kubwa ni kuzuia mashambulizi ya timu pinzani na kuanzisha mashambulizi.
Mara kadhaa Amrouche humuanzisha benchi na kumuingiza katikati ya kipindi cha pili kwa ajili ya kumsaidia mtangulizi wake ambaye aidha huwa ni Mudathir au Mzamiru Yassin au Sospeter Bajana kulingana na kikosi kilivyo siku hiyo.
Kiungo huyo wakati anajumuishwa na Amunike mwaka 2019 alikuwa akikipiga Petrojet FC ya huko huko Misri, kucheza kwake muda mrefu ligi ya Misri na kiwango anachoendelea kukionesha ni miongoni mwa vitu vilivyomshawishi Amrouche kumpa nafasi kwenye kikosi chake.
FEI TOTO
Hizi ni fainali za pili kwa kiungo huyu wa zamani wa JKU ya Zanzibar, ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango bora na utayari wa kutosha kuipigania Stars.
Hiyo inatokana na takwimu zake za mabao na pasi za mwisho za mabao kwenye Ligi Kuu NBC. Pamoja na hilo, Fei atarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa maingizo mapya ambayo nayo yameonesha uwezo mkubwa katika mechi za kirafiki na zile za kufuzu.
Fei Toto aliyejiunga na Azam FC akitokea Yanga hakuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi kilichoshiriki Afcon ya 2019.
Alikuwa na mchango mdogo kutokana na uchanga wake na kukosa uzoefu wa michuano mikubwa kama hiyo wakati ambao ndiyo kwanza alikuwa na msimu wa kwanza tangu ajiunge na Yanga akitokea JKU.
MSUVA
Kiwango chake na ubora wake hauna mashaka mbele ya Watanzania, ni miongoni mwa wachezaji wenye mchango mkubwa kwenye kikosi hicho ambacho hivi karibuni kimekuwa kikiundwa na nyota wengi kutoka ligi tofauti tofauti Afrika na kwingineko duniani.

Hiyo ni kutokana na mabao yake ambayo mara kadhaa yamekuwa yakiiweka timu hiyo katika nafasi nzuri kwenye mashindano tofauti.
Alikuwepo Misri na ndiye mchezaji aliyefunga bao la kwanza la Tanzania katika michuano hiyo dhidi ya Kenya, mechi iliyoisha kwa Stars kufungwa mabao 3-2.
Amrouche amempa nafasi nyingine ya kuipigania Tanzania kwenye ardhi ya gwiji Didier Drogba ingawa atakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa maingizo mapya kwenye eneo la ushambuliaji analocheza.
Wachezaji kama Kokola M’mombwa wa Macarthur ya Australia, Kibu Denis wa Simba na Samatta ni miongoni mwa wanaohatarisha nafasi ya Msuva lakini uzoefu mkubwa wa kucheza timu kama Wydad AC, Difaa El Jadida, Al-Quadsia kabla ya hivi karibuni kusitishiwa mkataba JS Kabylie, vinatosha kumpa mchezaji huyo wa zamani wa Yanga nafasi ya kutumainiwa tena msimu huu.
ZIMBWE JR
Pamoja ya kucheza mechi moja pekee dhidi ya Algeria kwenye michuano ya mwaka 2019, beki huyo wa kushoto wa kutumainiwa Simba amejumuihswa tena safari hii kwenda kuitetea Tanzania.
Zimbwe anatarajia upinzani mkubwa wa kupigania nafasi kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa wachezaji wengine kama Novatus Dismas wa Shaktar Donetsk ya Ukraine na Abdi Banda wa Richards Bay ya Afrika Kusini.

SAMATTA
Nahodha aliyeiongiza Stars kushiriki Afcon kwa mara ya pili. Ndiye kioo hasa cha taifa katika soka kutokana na mafanikio makubwa aliyonayo katika miaka ya hivi karibuni na kuweka rekodi lukuki katika ligi alizocheza Ulaya na Afrika akiwa na TP Mazembe takriban miaka minane iliyopita.
Uzoefu mkubwa alionao na uwezo wake wa kufumania nyavu ingawa kwa sasa anaonekana kupungua lakini ndivyo vinavyoendelea kumfanya avae jezi namba 10 katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Aliweka alama yake alipofunga bao moja tulipofungwa mabao 3-2 na Kenya mwaka 2019 na sasa ni wakati mwingine kudhihirisha kwa Watanzania kuwa bado ana umuhimu katika kikosi hicho kilichosheheni vijana wengi msimu huu kuliko vingine vinavyoshiriki michuano hiyo.
Bado hakuna mashaka makubwa juu yake katika umri wa miaka 31 alionao kwa mujibu wa makabrasha yake, ikitazamiwa pengine hii inaweza kuwa michuano yake ya mwisho kushiriki na Stars hivyo anapaswa kuonesha ukongwe na uongozi wake katika kipindi hiki kuliko vipindi vingine vyote vilivyopita na kuacha alama thabiti kwa vijana wanaofuata.