Rio de Janeiro, Brazil
Kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil, Dorival Junior (pichani) amesema Neymar ni kati ya wachezaji watatu bora duniani lakini kwa timu ya taifa ya Brazil inayopitia kipindi kigumu ijifunze kuishi bila ya mchezaji huyo majeruhi.
Dorival ambaye mwaka 2010 alitimuliwa katika klabu ya Santos baada ya kumuweka benchi Neymar, Jumatano iliyopita aliteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil akichukua nafasi ya kocha wa muda Fernando Diniz aliyetimuliwa.
Brazil kwa sasa haina mwenendo mzuri ikiwa kwenye mbio za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, tayari imepoteza mechi tatu kati ya sita ingawa mtihani wa kwanza kwa Dorival utakuwa Juni mwaka huu kwenye fainali za Copa America.
“Brazil lazima ijifunze kuangalia mbele bila ya kuwa na Neymar kwa sababu ni mchezaji majeruhi, tunaye (Neymar) mmoja wa wachezaji watatu bora duniani na hapo tutakuwa tukimtegemea yeye,” alisema Dorival.

Neymar ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya kuifungia timu ya Brazil mabao mengi, aliumia goti la mguu wa kushoto Oktoba mwaka jana wakati akiiwakilisha timu yake ya taifa na tayari amefanyiwa upasuaji akitarajiwa kurudi uwanjani Agosti mwaka huu.
Dorival alisema kwamba Neymar ni mchezaji muhimu sana kama tu atakuwa amepona na kuwa makini na alipoulizwa kama matatizo yao ya siku za nyuma yanaweza kuharibu uhusiano wao kwenye timu ya taifa, kocha huyo alijibu kwa kifupi, “Sina tatizo lolote na Ney.”
“Sijawahi kuwa na tatizo lolote na Neymar, bodi ya klabu ya Santos ilichukua uamuzi wa kunifukuza na niliheshimu hilo na hivyo ndivyo ilivyokuwa lakini sijawahi kuwa na tatizo na Neymar, kila wakati ninapokutana naye tunakuwa vizuri,” alisema Dorival.