London, England
Kocha wa zamani wa England ambaye pia ndiye kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu hiyo, Sven-Goran Eriksson (pichani) ametangaza kuwa na maradhi ya saratani (kansa).
Eriksson, 75, alikinoa kikosi cha England kwenye fainali za Kombe la Dunia 2002 na 2006 pamoja na fainali za Kombe la Ulaya 2004 ay Euro 2004 na katika michuano yote hiyo aliishia robo fainali.
“Nitajitahidi kukabiliana nayo kadri niwezavyo, nina maradhi na ni makubwa, nina hali mbaya, mbaya, ni vigumu kuzungumza kwa undani, na hivyo ni bora nisifikirie jambo hilo,” alisema Eriksson.
Eriksson, aligundulika kuwa na maradhi ya saratani mwaka mmoja uliopita na miezi 11 iliyopita alijiuzulu nafasi ya ukurugenzi wa michezo katika klabu ya Karlstad ya Sweden kwa kilichoelezwa kuwa ni matatizo ya kiafya.
“Bado naishi maisha ya kawaida, sipo hospitali, huwa naenda mara kadhaa lakini ninaishi nyumbani na nina marafiki hapa, Krismasi na Mwaka Mpya familia yote ilikuwa hapa, watu wengi walikuja,” alisema.
“Nitajitahidi kufanya mazoezi kwa wingi kadri iwezekanavyo jambo ambalo ni tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita ingawa naishi maisha ya kawaida,” alisema Eriksson.
“Unapopata ujumbe kama huo unashukuru kila siku na unakuwa mwenye furaha pale unapoamka asubuhi na kujiona upo sawa, kwa hiyo hilo ndilo ninalofanya,” alisema.
“Nilijiona mkamilifu kiafya lakini ghafla nikapata kiharusi, tatizo halikuwa kwa kiwango kikubwa, kwa hiyo nilianguka na watoto wangu wakanipeleka hospitali,” alisema.
“Baada ya vipimo vya siku moja wakaniambia kuhusu kiharusi lakini wakasema si tatizo, utapona kwa asilimia 100 lakini kibaya zaidi waliniambia nina saratani na hawawezi kunifanyia operesheni,” alisema Eriksson.
“Waliniambia watanipa tiba na dawa ili niweze kuishi kwa muda mrefu kadri iwezekanavyo, nina tatizo hilo na hawawezi kunifanyia operesheni,” alisema Eriksson.
Nahodha wa zamani wa England, Wayne Rooney akitumia mtandao wa Twitter au X alisema, “habari ya kusikitisha, tuko pamoja kifikra na Sven Goran-Eriksson na familia yake, kocha bora na mtu wa kipekee, aliyependwa na kuheshimiwa na kila mtu, sote tuko pamoja nawe Sven, endelea kujipigania.”