Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Prisons, umesema hauna mpango wa kumuuza mshambuliaji wao, Edwin Balua kutokana na kuhofia kukosa mbadala wake katika kipindi hiki cha dirisha dogo.
Mtendaji Mkuu wa Prisons, Ajabu Kifukwe amesema leo Alhamisi kuwa hiyo ni kutokana na malengo makubwa waliyokuwa nayo kwa mchezaji huyo ambaye pia bado wana mkataba naye wa muda mrefu.
“Hatuna mpango wa kumuuza Balua, bado yupo kwenye mipango ya kocha wetu Hamad Ally, ni mchezaji mwenye mchango mkubwa hivyo hatuwezi kumuachia sababu hatuwezi kuuza silaha muhimu wakati ukiangalia bado hatujawa na matokeo mazuri sana kwenye ligi,” alisema Kifukwe.
Kiongozi huyo alisema taarifa za Simba kumuhitaji mchezaji huyo wamekuwa wakizisikia kwenye vyombo vya habari na hakuna kiongozi yeyote wa timu hiyo aliyefika ofisini kwao lakini hata akijitokeza hakuna biashara hiyo kwa sasa.
Kiongozi huyo alisema wanatambua mpira ni biashara lakini kwa kipindi hiki ni vigumu kumruhusu mchezaji kama huyo kuondoka na kama kweli Simba wanamuhitaji basi wasubiri mkataba wake utakapomalizika, vinginevyo wanapaswa kuheshimu mkataba.
Balua amekuwa na mwanzo mzuri tangu kuanza kwa msimu huu na tayari ameifungia timu yake mabao manne ikiwemo lile aliloifunga Simba wakati timu hizo zilipokutana Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Soka Prisons hawampigi bei Balua
Prisons hawampigi bei Balua
Read also