Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola amekiri kwamba pamoja na kutinga fainali Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Singida Fountain Gate, mchezo ulikuwa mgumu na iliwabidi kutumia mbinu na uzoefu wa wachezaji wao kushinda.
Simba ililazimika kusubiri mikwaju ya penalti ili kujihakikishia kucheza fainali baada ya kutanguliwa kufungwa bao la mapema na wapinzani wao hao kabla ya kusawazisha dakika ya mwisho na kufanya matokeo kuwa sare ya 1-1 kwenye dakika za kawaida.
Matola alisema ulikuwa mchezo mgumu ambao uliwalazimu kubadili mifumo ya uchezaji mara tatu lakini anawapongeza wachezaji wake kwa kutokata tamaa na kusawazisha bao hilo ‘jioni’.
“Kipindi cha pili tulirudi vizuri na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Singida, kiukweli ilitusaidia na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika za mwisho lakini ukweli mchezo ulikuwa mgumu na hiyo ni kutokana na ubora wa wapinzani,” alisema Matola.
Kocha huyo alisema kipindi cha kwanza kilikuwa bora kwa Singida ambao walicheza vizuri kwa dakika 15 hadi 20, baada ya hapo walirudi nyuma kujihami kitu kilichowapa nguvu ya kuendelea kupambana na anashukuru iliwalipa.
Nahodha wa Singida, Gadiel Michael alimtupia lawama mwamuzi aliyechezesha mchezo huo kwa kushindwa kutenda haki katika baadhi ya maamuzi ikiwemo mpira wa kona ambao ulizaa bao la kusawazisha la Simba.
Beki huyo alisema hata dakika ambazo ziliongezwa pia zilishakamilika lakini anashangaa mwamuzi huyo aliendelea kuchezesha hadi pale Simba waliposawazisha ndio alimaliza mchezo.
“Kama walikuwa wanataka Simba aingie fainali wangetuambia tusije uwanjani kuliko hiki alichofanya mwamuzi, ni uonevu na siyo kitendo cha kiungwana,” alisema Gadiel.