Paris, Ufaransa
Matarajio ya Real Madrid kumsajili mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe huenda yakakwama baada ya rais wa PSG, Nasser Al Khelaïfi (pichani) kudai kwamba anataka mchezaji huyo abaki katika klabu hiyo.
Real Madrid na Liverpool zimekuwa mstari wa mbele kumtaka Mbappe huku Real Madrid ikionekana kuwa katika nafasi nzuri ya kumpata hasa baada ya mchezaji huyo kudaiwa kusema kwamba yuko tayari kwenda Madrid.
Liverpool nayo haipo nyuma katika hilo ikidaiwa kumuingiza katika hesabu zake mshambuliaji huyo hasa baada ya kuwapo habari kwamba mshambuliaji wao tegemeo, Mohamed Salah huenda akatimkia Saudi Arabia.
Kauli ya Al Khelaïfi kumtaka Mbappe abaki katika timu hiyo licha ya mkataba wake wa sasa kufikia ukomo Juni mwaka huu inakuwa pigo kubwa kwa klabu hizo mbili katika dhamira yao ya kumpata mshambuliaji huyo.
“Angalia, sijaribu kuficha chochote, nataka Kylian Mbappe abaki hapa PSG. Ni mchezaji bora duniani na klabu bora kwake ni PSG, yeye ni nguzo muhimu katika mpango kazi wetu,” alisema Al Khelaïfi.
Habari za ndani zinadai kwamba Mbappe mwenyewe amepanga kuweka wazi hatma yake wiki chache zijazo lakini kilicho wazi ni kwamba kama mpango wa kubaki utakwama chaguo lake litakuwa kati ya Real Madrid au Liverpool.
PSG imedhamiria kumbakisha Mbappe ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji bora katika klabu hiyo ingawa mshambuliaji huyo amewahi kuelezea nia yake ya kutaka changamoto mpya nje ya klabu hiyo na hapo hapo atakuwa huru kuamua lolote mkataba wake na PSG utakapofikia mwisho.