Na mwandishi wetu
Bao la dakika za nyongeza limeiwezesha Simba kupata sare ya 1-1 dhidi ya Singida Fountain Gate katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na hatimaye kumalizia na ushindi wa penalti 3-2 na kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Simba na Singida FG zimeumana hii leo Jumatano usiku katika mechi kali ambayo mashabiki wengi waliamini Simba ingetolewa na Singida baada ya kuhaha kwa muda wa takriban dakika 80 kusaka bao la kusawazisha ambalo hatimaye walilipata na kuzifanya timu hizo zipigiane penalti.
Katika mikwaju ya penalti waliofunga kwa upande wa Simba ni Luis Miquissone, Israel Mwenda na Mosses Phiri wakati kwa Singida waliofunga ni Abuya na Deus Kaseke.
Waliokosa kwa Simba ni Shomary Kapombe na Saido Ntibazonkiza ambaye licha ya kusifika kwa umahiri kwenye mikwaju ya penalti lakini leo shuti lake liligonga mwamba wa juu na kutoka nje.
Kwa upande wa Singida waliokosa ni Gadiel Michael na Hamad Waziri ambaye licha ya kumchambua kipa wa Simba, Ally Salim lakini kipa huyo aliokoa shuti lake la chinichini kwa kutumia miguu.
Mpigaji mwingine wa Singida aliyekosa penalti ni Meddy Kagere ambaye licha ya kuonesha ufundi wa kutaka kumchanganya kipa wa Simba lakini mwishowe alipiga shuti hafifu lililodakwa na kipa huyo.
Katika dakika 90 za kawaida, Singida ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 11 mfungaji akiwa ni Elvis Rupia ambaye alineemeka na makosa ya beki wa Simba, Kennedy Juma.
Beki huyo akiwa karibu kabisa na lango la timu yake alitoa pasi kwa mchezaji wa Singida ambaye alimuunganishia mfungaji na kuipa Singida bao hilo la mapema.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilianza kupambana ikisaka bao la kusawazisha lakini ukuta mgumu wa Singida FG ulikuwa mara kwa mara ukivuruga mashambulizi ya Simba yaliyotokea zaidi upande wa kushoto na kulia.
Hatimaye katika dakika sita za nyongeza, Simba walipata kona iliyotokana na mpira uliopigwa na Saidoo na kumkuta Ngoma aliyeujaza mpira wavuni na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Simba.
Kona hiyo hata hivyo iligomewa na wachezaji wa Singida kwa kumzonga mwamuzi ambaye alisimamia msimamo wake wa kutaka kona ipigwe.
Katika vurugu hizo ilibidi nguvu ya ziada kutoka nje kwa msaada wa baadhi ya wachezaji wa Singida na hatimaye hali ikatulia na timu kuanza kupigiana penalti na Simba kutoka na ushindi.
Kwa ushindi huo Simba sasa inasubiri kucheza mechi ya fainali na Mlandege hapo Jumamosi, Mlandege ilishinda nusu fainali nyingine dhidi ya APR ya Rwanda.
Soka Penalti zaibeba Simba Mapinduzi Cup
Penalti zaibeba Simba Mapinduzi Cup
Read also