Na mwandishi wetu
Winga wa timu ya FAR Rabat ya Morocco, Bernard Morrison amesema bado anapambana kupata uraia wa Tanzania ili kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’.
Mchezaji huyo mwenye vituko amewahi kutamba nchini akiwa na klabu kubwa za Yanga na Simba, kabla ya msimu huu kutimkia Morocco.
Akizungumza na mmoja wa wahamasishaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Nicky Reynold ‘Bongo Zozo’ mchezaji huyo ambaye kwa sasa yupo nchini kwao Ghana akiuguza majeraha alisema ameshazungumza na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ kuhusu suala hilo la kubadili uraia.
“Ukweli napenda sana kuishi Tanzania, watu wake ni wakarimu na wana upendo sana. Nimezungumza na MwanaFA kuhusu kubadili uraia na yeye ameniambia analishughulikia suala langu kwa hiyo bado nasubiri,” alisema Morrison.
Mchezaji huyo pia alisema kutokana na kuishi vizuri na Watanzania anafikiria kurudi kucheza tena ligi ya Tanzania pindi mkataba wake na FAR Rabat utakapomalizika.
Kwa muda mrefu tangu akiwa nchini akiichezea Simba, Morrison alianza mchakato huo wa kuomba uraia ili kuitumikia Stars na hiyo ni baada ya kutojumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa lake la Ghana ‘Black Star’ kilichoshiriki Kombe la Dunia 2022.