Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Jonas Mkude amesema tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu aliyoipata kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KVZ itabadilisha mtazamo wa watu wengi dhidi yake.
Mchezaji huyo alisema watu wengi wamekuwa na mtazamo hasi juu yake kwamba ni mtu asiye na nidhamu kitu ambacho siyo kweli.
“Kwanza namshukuru kocha wangu Miguel Gamondi kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza mechi hizi za Kombe la Mapinduzi na tuzo hii itanisaidia kuondoa mawazo mabaya waliyokuwa nayo baadhi ya watu juu yangu kwamba sina nidhamu,” alisema Mkude.
Kiungo huyo ambaye ametua Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Simba, alisema siku zote yeye ni mtu anayezingatia nidhamu, iwe ndani au nje ya uwanja na hata shutuma ambazo amewahi kupewa huko nyuma mara nyingi zimekuwa na mrengo wa kumchafua.
Alisema mara nyingi huwa anapenda kukaa kimya akiamini ipo siku ukweli utajulikana na tuzo hiyo imedhihirisha kwamba yeye ni mtu wa aina gani.
Mkude ambaye pia katika mchezo huo ulioisha kwa suluhu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, alivaa kitambaa cha unahodha, amesema ataendelea kujitumia kuipigania timu hiyo kubeba ubingwa wa michuano hiyo ambayo kwa sasa ipo hatua ya robo fainali.