Rio de Janeiro, Brazil
Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Mario Zagallo mwenye rekodi ya kubeba Kombe la Dunia mara nne akiwa kocha na mchezaji wa timu hiyo, amefariki dunia akiwa na miaka 92.
Zagallo, kabla ya kuingia katika ukocha alikuwa mchezaji akicheza nafasi ya winga ambapo akiwa na kikosi cha Brazil walifanikiwa kubeba Kombe la Dunia mwaka 1958 na 1962.
Baada ya hapo, Zagalo alikuwa kocha wa timu hiyo, akiwa na kikosi kinachotajwa kuwa bora kikiwa na wachezaji mastaa kina Pele, Carlos Alberto, Jairzinho na wengineo ambao walibeba Kombe la Dunia mwaka 1970.
Baada ya mataji hayo, Zagallo aliibuka katika timu hiyo mwaka 1994 akiwa kocha msaidizi wa Carlos Alberto Parreira, timu ambayo pia ilibeba Kombe la Dunia nchini Marekani na hilo kuwa taji la nne kwa Zagallo.
Zagallo kwa mara nyingine alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu ya Brazil akiwa kocha mkuu na mwaka 1998 aliifikisha timu hiyo hatua ya fainali ya Kombe la Dunia nchini Ufaransa lakini ilikwama mbele ya wenyeji waliobeba taji hilo.
Mafanikio hayo yamemfanya Zagallo kuwa mtu wa kwanza duniani mwenye rekodi ya kubeba Kombe la Dunia akiwa mchezaji na baadaye kocha, rekodi ambayo baadaye iliwekwa na Franz Beckenbauer wa Ujerumani na Didier Deschamps wa Ufaransa.
Akizungumzia msiba wa gwiji huyo wa soka, rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva alisema Zagallo alikuwa mmoja wa wanasoka na makocha bora wa wakati wote.
“Ni mfano wa Mbrazili ambaye hakuwahi kuwa mwenye kukata tamaa, ni hulka yake ya kujitoa, kupigania jambo kwa mahaba ndicho kitu anachotuachia katika nchi yetu yote na dunia ya soka kwa ujumla,” alisema Rais Da Silva.
Brazil hadi sasa ndiyo nchi yenye mafanikio zaidi katika soka ikiwa imebeba Kombe la Dunia mara tano na Zagallo ni mmoja wa wanasoka na makocha mahiri aliyehusika kufanikisha historia hiyo ya kipekee.
Katika mahojiano aliyowahi kufanya wakati wa uhai wake, Zagallo alikumbushia tukio la fainali za Kombe la Dunia mwaka 1950 akiwa miongoni mwa watu takriban 200,000 kwenye Uwanja wa Maracana walioshuhudia wenyeji Brazil wakibwagwa na Uruguay katika mechi ya fainali.