Roma, Italia
Kocha wa Roma, Jose Mourinho amesema hajawasiliana na Shirikisho la Soka Brazil (CBF) kwa ajili ya kupewa kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Brazil kuanzia Julai mwaka huu.
CBF kwa sasa wapo katika mchakato wa kumsaka kocha wa kudumu atakayechukua nafasi ya kocha wa muda wa timu hiyo, Fernando Diniz ambaye mkataba wake unafikia ukomo Juni mwaka huu.
Baada ya kocha aliyetajwa kuwa chaguo la kwanza la Brazil, Carlo Ancelotti kuamua kuongeza mkataba wa kuinoa Real Madrid hadi Juni 2026, habari zilidai kwamba mabosi CBF waliwasiliana na wakala wa Mourinho, Jorge Mendes kuulizia uwezekano wa kumpata kocha huyo.
“Sijui kama ni kweli Brazil wananitaka mimi, hawajazungumza na mimi, nilimuombataka wakala wangu kutozungumza lolote kuhusu mikataba yangu,” alisema Mourinho.
Rais wa CBF, Ednaldo Rodrigues aliwahi kunukuliwa akisema kwamba jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha timu ya taifa ya Brazil inakuwa na kocha wa kudumu na pia zipo habari kwamba mmoja wa makocha anaowapigia hesabu ni Dorical Junior wa timu ya Sao Paulo ya Brazil.
Mourinho amekuwa kocha wa Roma tangu mwaka 2021 na mkataba wake wa sasa na klabu hiyo unafikia ukomo Juni 30 mwaka huu na hajawahi kusema lolote kuhusu mambo yake ya baadaye pindi mkataba huo utakapomalizka,
Mourinho ambaye pia amewahi kuzinoa timu za FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Man United na Tottenham, amewahi kukataa ofa za kuwa kocha wa timu za taifa za Ureno na Saudi Arabia.