Na mwandishi wetu
Beki wa kati wa Simba, Che Malone Fondoh (pichani) amesema hana ugomvi na kipa wa timu hiyo, Ally Salim juu ya kilichotokea jana Alhamisi katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Singida Fountain Gate ni kutimiza majukumu ya timu.
Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 2-0, lakini kutokana na presha ya mchezo huo kipa huyo alionekana kumsukuma beki huyo mara mbili katika dakika ya 65 kutokana na makosa aliyoyafanya na kukaribia kuwapa wapinzani wao bao.
Akizungumza leo Ijumaa kuhusu tukio hilo, Che Malone alisema kilichotokea ni kukumbushana na kuongeza umakini sababu ulikuwa mchezo mgumu kutokana na malengo waliyonayo ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
“Hatuna ugomvi na Ally, vile ni vitu vya kawaida kutokea ndani ya uwanja, tulikuwa tunakumbushana, unajua presha ilikuwa kubwa na timu tuliyokuwa tunacheza nayo ilikuwa inahitaji kuweka heshima dhidi yetu,” alisema Che Malone.
Beki huyo aliyejiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coton Sport ya kwao Cameroon alisema haoni sababu ya kulikuza jambo hilo kwani baada ya mchezo walizungumza na kulimaliza wakiwa palepale uwanjani
Simba inatarajia kukamilisha mechi za hatua ya makundi kwa kucheza na APR ya Rwanda ikiwa hadi sasa imeruhusu bao moja katika mechi mbili ilizocheza kwenye michuano hiyo ambayo kilele chake ni Januari 13, mwaka huu.