Birmingham, England
Wayne Rooney amefutwa kazi Birmingham City baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi 15 na kupoteza tisa kati ya hizo hali ambayo imeiweka timu hiyo katika hatari ya kushuka daraja.
Birmingham inamilikiwa na Wamarekani wa kampuni ya Knighthead Capital Management, inacheza ligi ya Championship na kwa hali ilivyo haitoshangaza ikishuka daraja msimu huu wa 2023-24.
Uamuzi wa kumtimua Rooney ulifikiwa leo Jumanne chini ya mmoja wa mabosi na mwanzilishi wa kampuni hiyo, Tom Wagner baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-0 na Leeds United siku ya mwaka mpya.
Taarifa ya kumfuta kazi Rooney iliyotolewa leo ilieleza, “Birmingham City leo imeamua kuachana na kocha Wayne Rooney pamoja na kocha wa kikosi cha pili, Carl Robinson.
“Licha ya juhudi zao matokeo hayakuwa yenye kukidhi matarajio ambayo yaliwekwa wazi, kwa hiyo bodi imeona mabadiliko ya uongozi ni jambo zuri katika soka la klabu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Klabu hiyo katika taarifa hiyo pia iliwashukuru Rooney na Robinson kwa wakati ambao wamekuwa na timu hiyo na imemteua Steve Spooner aliyekuwa msimamizi wa maendeleo ya soka katika klabu hiyo kuwa kocha wa muda.
Habari za ndani pia zinadai kuwa nafasi ya ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Garry Cook ambaye ofisi yake ilihusika kumpa ajira Rooney kwa kumsainisha mkataba wa miaka mitatu na nusu, naye huenda akafutwa kazi.
Rooney nyota wa zamani wa Man United na timu ya taifa ya England, alijiunga na Birmingham Oktoba baada ya kuacha kazi katika klabu ya D.C. United ya Marekani aliyokuwa akiinoa.
Baadhi ya mashabiki Birmingham walianza kumzomea Rooney ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Everton wakimwambia wazi kwamba anatimuliwa kazi mapema.