Na mwandishi wetu
Licha ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKU kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, kocha mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha amesema hajaridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na safu yake ya ulinzi.
Ushindi huo wa jana Jumatatu umeifanya Simba kufikisha pointi tatu na kushika nafasi ya pili kwenye kundi B nyuma ya vinara Singida Fountain Gate wenye pointi sita ambao tayari wamefuzu robo fainali na kuungana na Mlandege na Azam FC.
Benchikha raia wa Algeria alisema ni ushindi muhimu kwao, walihitaji kuanza mashindano vizuri lakini makosa yaliyofanywa na safu yake ya ulinzi hayajamfurahisha.
“Sijaridhishwa na kiwango cha wachezaji kutokana na makosa yaliyofanywa na safu ya ulinzi, sisi ni timu kubwa yenye wachezaji wakubwa hatuwezi kufanya makosa ya namna ile.
“Tuliruhusu bao moja lakini wapinzani wetu wakapoteza nafasi nyingine mbili, tumefanya makosa kama wangekuwa makini wangetuadhibu lakini tunashukuru kwa pointi tatu tunarudi kurekebisha makosa na kujipanga na mchezo ujao,” alisema Benchikha.
Katika hatua nyingine Benchikha alisema amevutiwa na uwezo uliooneshwa na mchezaji mpya, Salehe Karabaka ambaye ameanza vyema kwa kufunga bao kwenye mchezo huo.
“Unapocheza mchezo wa kwanza na kufunga baada ya dakika mbili ni jambo zuri, nimefurahishwa naye (Karabaka) na ana kesho iliyo bora na tuko hapa kwa ajili ya kumsaidia kiufundi ili aweze kufika mbali,” alisema Benchikha.