Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Azam FC, Yossouf Dabo amesema ujio wa mshambuliaji, Franklin Navarro (pichani) utaisaidia timu hiyo kutimiza kwa haraka malengo yao waliyokusudia kuyafikia msimu huu.
Kocha huyo alisema alikuwa akimfuatilia kwa muda mrefu mshambuliaji huyo raia wa Colombia na aliushawishi uongozi wa timu hiyo kumsajili akiamini ujio wake utainufaisha timu yake.
“Nina imani kubwa na Franklin, ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga, uwepo wake pamoja na washambuliaji waliopo hivi sasa wakiongozwa na Prince Dube na Feisal Salum, uwezekano wa kutwaa ubingwa msimu huu ni mkubwa,” alisema Dabo.
Dabo alisema ujio wa Navarro utaongeza pia ushindani kwa washambuliaji waliopo kwenye timu hiyo ambao mpaka sasa tayari wamefunga mabao 35 katika michezo 13 ya Ligi Kuu NBC.
Dabo alisema baada ya Navarro, kuna wachezaji wengine wawili wamekusudia kuwaongeza ili kuzidi kukiimarisha kikosi chao kwa lengo la kubeba ubingwa wa ligi kuu na michuano mingine ya ndani.
Tayari Navarro amejiunga na Azam iliyopo visiwani Zanzibar ikishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi na leo Jumamosi majira ya saa 2.15 usiku timu hiyo inatarajia kucheza na Chipukizi United.
Soka Dabo ampamba straika mpya Azam
Dabo ampamba straika mpya Azam
Read also