Manchester, England
Kipa wa Man United, Andre Onana anadaiwa kuanza mazungumzo na mabosi wa soka wa Cameroon ili achelewe kadri iwezekanavyo kujiunga na timu ya taifa kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Onana yumo ndani ya kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kinachojiandaa na fainali za Afcon zitakazoanza kutimua vumbi Januari 13 mwakani nchini Ivory Coast na kufikia tamati Februari 11.
Awali Onana alisema yupo tayari kuiwakilisha Cameroon kwenye fainali hizo lakini habari za ndani zinadai kwamba kipa huyo anachotaka ni kuhakikisha anachelewa kuondoka Man United.
Katika maandalizi yake ya Afcon, Cameroon inatarajia kuweka kambi Saudi Arabia na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Zambia, mechi ambayo itapigwa Januari 9 mwakani.
Baada ya kutambua ratiba hiyo, Onana anahaha kuhakikisha anaiwakilisha Man United katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Wigan, mechi ambayo itapigwa Januari 8 mwakani.
Kwa maana hiyo, Onana ni kama vile yuko tayari kuikosa mechi na Zambia badala yake anachotaka ni kuwa na timu hiyo kwenye mechi ya kwanza ya Afcon dhidi ya Guinea, mechi itakayochezwa Januari 15 mwakani.
Januari 14 mwakani, Man United itakuwa na mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Tottenham na Januari 27, siku ambayo mechi za hatua ya mtoano za Afcon zitaanza, Man United huenda ikawa uwanjani siku hiyo katika mechi nyingine ya Kombe la FA.
Baada ya hapo Man United itakuwa na mechi nyingine za EPL, Februari Mosi dhidi ya Wolves, Februari 4 dhidi ya West Ham na Februari 11 dhidi ya Aston Villa.
Suala la Onana kuchelewa kujiunga na timu ya Cameroon kama likiwezekana bado atazikosa mechi kadhaa za Man United vinginevyo ataziwahi iwapo Cameroon itatolewa mapema tofauti na hivyo nafasi yake atapewa kipa namba mbili wa Man United, Altay Bayindir.
Suala la Onana huenda pia likaibua utata na kocha wa Cameroon, Rigobert Song ambaye amemuacha katika timu hiyo mshambuliaji wa Bayern Munich, Eric-Maxim Choupo Moting baada ya mchezaji huyo kukosekana katika mechi tatu zilizopita.
Wakati wa fainali za Kombe la Dunia za Qatar zilizofanyika Novemba na Desemba mwaka 2022, Onana alitangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Cameroon kabla ya kubadili uamuzi huo Septemba mwaka huu.
Katika Afcon, Cameroon imepangwa Kundi C na baada ya mechi yake na Guinea itakuwa na kibarua kingine dhidi ya mabingwa watetezi Senegal na kumalizia mechi za makundi kwa kuumana na Gambia.
Kikosi kamili cha Cameroon ni kama ifuatavyo: Makipa, Andre Onana (Man United), Devis Epassy (Abha Club), Simon Ngapandouetnbu (Marseille) na Fabrice Ondoa (Nimes)
Mabeki: Oumar Gonzalez (Al Raed), Harold Moukoudi (Athens), Tolo Nouhou (Seattle Sounders), Junior Tchamadeu (Stoke City), Enzo Tchato (Montpellier), Darling Yongwa (Lorient) Malcom Bokele (Bordeaux), Christopher Wooh (Stade Rennais) na Jean-Charles Castelletto (Nantes),
Viungo: Olivier Ntcham (Samsunspor), Wilfried Nathan Doualla (Victoria United), Ben Elliott (Reading), Olivier Kemen (Kayserispor), Andre-Frank Zambo Anguissa (Napoli) na Yvan Neyou (Leganes),
Washambuliaji: Francois-Regis Mughe (Marseille), Vincent Aboubakar (Besiktas), Leonel Ateba (Dynamo Douala), Frank Magri (Toulouse), Faris Pemi Moumbagna (Bodo/Glimt), Georges-Kevin Nkoudou (Damac), Karl Toko Ekambi (Abha Club) na Clinton Njie (Sivasspor).
Kimataifa Onana ajipanga kuchelewa Afcon
Onana ajipanga kuchelewa Afcon
Read also