Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda amesema baada ya kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake, mipango na nguvu zao sasa ni katika mechi ijayo na watani zao wa jadi, Yanga Princess itakayochezwa Januari 3, mwakani.
Simba Queens ilirejea kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 jana Alhamisi dhidi ya Baobab Queens katika mchezo wa pili ya ligi hiyo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mgunda alisema licha ya ushindi huo mnono ameona mapungufu kadhaa kwenye kikosi chake na atayafanyia kazi mazoezini kuyaondoa na kuhakikisha wanaimarika katika ubora wao.
“Na pia mechi ijayo ni ‘derby’ lazima tujipange vizuri, tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kurekebisha makosa kadhaa ili kuhakikisha tunapata pointi tatu kwenye kila mechi ili kufikia malengo yetu,” alisema Mgunda.
Yanga Princess iliyoibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Amani Queens, inashikilia nafasi ya pili kwa pointi sita kama kinara Simba kama JKT Queens na Alliance Girls zinazoshika nafasi ya tatu na nne, zikipishana kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.