Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imekusudia kuwashangaza mashabiki wao wa visiwani Zanzibar kwa kutambulisha baadhi ya nyota wapya iliyowasajili kwenye dirisha dogo kwa lengo la kuwaongezea nguvu katika mashindano wanayoshiriki msimu huu.
Kwa mujibu wa maelekezo ya kocha wao Miguel Gamondi, timu hiyo imepanga kusajili wachezaji watatu wapya kwenye dirisha dogo kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake na miongoni mwa nafasi ambazo amekusudia kuziimarisha ni ushambuliaji, kiungo mkabaji na beki wa kati.
Meneja wa Yanga, Walter Harrison alisema uongozi wao umepanga kuwashangaza mashabiki zao wa Zanzibar kwa kutambulisha baadhi ya wachezaji waliowasajili kwenye dirisha dogo kutokana na kuthamini mchango wao.
“Bado sijajua idadi ya wachezaji ambao wamesajiliwa lakini Rais Hersi Saidi ameniambia anataka kuwashangaza mashabiki wetu kwa kutambulisha baadhi ya wachezaji wapya tukiwa kwenye michuano ya Mapinduzi, Zanzibar,” alisema Walter.
Walter alisema wanakwenda Zanzibar wakiwa wamejipanga kuwapa burudani mashabiki zao ikiwemo kupambana kubeba ubingwa wa michuano hiyo inayoanza kutimua vumbi Alhamisi hii.
Mpaka sasa Yanga imemtambulisha kiungo mkabaji Shekhani Abdallah kutoka JKU ya Zanzibar akitarajiwa kuonesha zaidi uwezo wake kabla ya kurejea kwenye Ligi Kuu NBC na michuano ya kimataifa.