Barcelona, Hispania
Mshambuliaji Mbrazili, Vitor Roque (pichani) hatimaye amekamilisha taratibu za kujiunga na klabu ya Barcelona Jumatano hii na anatarajia kuanza mazoezi na kikosi cha kwanza cha timu hiyo keshokutwa Ijumaa.
Usajili wa mchezaji huyo kutoka klabu ya Athletico-PR ya Brazil umefikia hatua nzuri ambapo Barca italipa kiasi cha Dola 43.6 milioni hadi kukamilisha usajili huo.
Msimu wa usajili nchini Hispania unafunguliwa rasmi Januari 2 na baada ya taratibu zote kukamilika kwa asilimia 100, Roque huenda akaonekana rasmi katika kikosi cha timu hiyo Januari 4 katika mechi dhidi ya La Palmas.
Makubaliano ya Barça na Athletico kumsajili Roque yalifikiwa mwezi Julai mwaka huu ambapo mchezaji huyo alikubali kusaini mkataba wa kumfanya aichezee Barca kwa miaka saba.
Kanuni ya matumizi ya fedha katika klabu Ulaya imewaweka katika wakati mgumu Barca kufanya usajili na awali Roque alitarajiwa kujiunga na klabu hiyo kwa ajili ya msimu wa 2024-25.
Janga la majeruhi linaloiandama Barca na tatizo linaloonekana katika safu ya ushambuliaji, limeifanya klabu hiyo kuelekeza nguvu zake kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 18.
Roque kwa mara ya mwisho aliichezea Athletico, Desemba 3 na anaiacha klabu hiyo akiwa na rekodi ya kuifungia mabao 28 katika mechi 80.
Kati ya mabao hayo kwa mwaka 2023, Roque ameifungia timu hiyo mabao 21 katika mechi 44 kabla ya kuumia goti mwezi Septemba na kujikuta akisugua benchi kwa miezi miwili.
Jumamosi mchezaji huyo anatarajia kutangazwa kwa kuoneshwa kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki katika Uwanja wa Johan Cruyff, tukio ambalo litakuwa la pili kwake kuwa pamoja na wachezaji wenzake.