Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Simon Msuva amesema mechi yao dhidi ya Zanzibar Heroes ilikuwa ni kipimo kizuri kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) itakayofanyika Ivory Coast, mwakani.
Msuva amesema hayo baada ya mechi baina ya timu hizo iliyopigwa jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar na kuisha kwa sare ya 0-0, ikiwa ni mechi maalum ya ufunguzi wa uwanja huo baada ya kukarabatiwa kisasa.
“Kwanza tunashukuru mchezo ulikuwa mzuri, tunawashukuru Wazanzibari kwa ukarimu wao, tunamshukuru Rais wa Zanzibar (Hussein Mwinyi) Rais Mama Samia (Suluhu) kwa kutupa hamasa na kuweka hiki kitu, kwa upande wetu tumefurahi na mechi ilikuwa nzuri.
“Kipimo kilikuwa kizuri sababu wapo wengine hawajaripoti na sisi wengine ambao tupo tumewakilisha lakini kipimo kizuri kwa maandalizi ya Afcon na mwalimu kuna vitu ameviona, nafikiri tuendelee kuungana na tuendelee kupambana sababu hii ndio timu yetu ya taifa,” alisema Msuva.
Stars itakayoweka kambi nchini Misri kwa ajili ya kujiandaa na Afcon ni miongoni mwa timu 24 zitakazopambana kwenye michuano hiyo huku ikiwa ni timu pekee kutoka Afrika Mashariki.