Manchester, England
Hali ya mshambuliaji tegemeo wa Man City, Erling Haaland bado si nzuri ingawa kocha wake, Pep Guardiola ana matumaini ya mchezaji huyo kurudi uwanjani kabla ya mwisho wa mwezi Januari.
Pep alisema kwa sasa Haaland bado hajaweza hata kufanya mazoezi na wachezaji wenzake kutokana na majanga ya majeraha ya mguu ambayo yamekuwa yakimuandama katika siku za karibuni.
Hadi sasa Haaland amekosa mechi sita za Man City katika mashindano yote ikiwamo ya jana Jumatano alipokuwa nje ya uwanja akiwashuhudia wenzake wakitoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Everton katika Ligi Kuu England (EPL).
Picha ya hivi karibuni ya kwenye mitandao ya kijamii ya Man City ilimuonesha Haaland akichezea mpira wakati timu hiyo ikiwa Saudi Arabia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu na kuibua matumaini kwamba ameanza kuwa fiti lakini kiuhalisia hali yake bado si nzuri.
“Haaland anafanya mazoezi peke yake, hajumuiki na wachezaji wenzake kwenye timu, Kevin (De Bruyne) yeye ameanza mazoezi na wenzake lakini si Haaland, kwake bado ni suala la lini maumivu yataondoka,” alisema Pep.
“Tuna matumaini atakuwa amepona katika kipindi cha Januari lakini tatizo la kwenye mifupa bado ni kubwa, tatizo lake si kama la Phil Foden, tatizo la Erling ni kubwa,” alisema Pep.
Kuhusu De Bruyne ambaye hakuichezea timu hiyo tangu aumie misuli katika mechi ya kwanza ya msimu huu wa EPL dhidi ya Burnley, kwa sasa anaendelea vizuri na huenda Januari 6 akawa uwanjani katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Huddersfield Town.