Na mwandishi wetu, Zanzibar
Timu za Zanzibar Heroes na Kilimanjaro Stars zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya kirafiki ya uzinduzi wa Uwanja wa Amaan, Unguja, Zanzibar iliyochezwa Jumatano hii usiku.
Ikiwatumia wakali wake wanaocheza katika Ligi Kuu NBC, Zanzibar Heroes iliuanza mchezo huo kwa kasi katika dakika 20 za mwanzo ambapo Kili Stars walikuwa na kazi ya kuzuia mashambulizi.
Dakika ya kwanza tu ya mchezo huo, Baraka Mtui aliunasa mpira uliotokana na ushirikiano wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mudathir Yahya na akiwa karibu na eneo la 18 alifumua shuti la juu ambalo lilitoka nje ya lango na kumfanya kipa wa Kili Stars, Aishi Manula kuufuata kwa namna ya kuushuhudia mpira huo ukitoka nje.
Baada ya kushambuliwa, Kili Stars ilijibu mapigo kwa kuonesha uhai kuanzia dakika ya 21 kwa kufanya shambulizi la kwanza lililoongozwa na Simon Msuva ambaye aliambaa na mpira kwa kasi lakini shuti alilopiga halikuzaa matunda.
Dakika nane baadaye Msuva kwa mara nyingine aliunasa vizuri mpira wa juu lakini wakati akitaka kuelekea kwenye lango la Heroes, beki kisiki wa Heroes, Ibrahim Baca alimdhibiti vyema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.
Kipindi cha pili kocha wa Kili Stars Juma Mgunda aliwaingiza Muzamir Yassin, Kibu Denis, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ Sospeter Bajana na Abdul Sopu ambao waliiongezea uhai timu hiyo na kuanza kulisakama lango la Heroes.
Heroes ambao walianza kusumbuliwa na Kili Stars nao dakika ya 51 walionesha uhai baada ya Fei Toto kumpenyezea pasi ya chinichini Maabad Maulid ambaye alifumua shuti lakini lilitoka nje ya lango.
Kili Stars iliendelea kulisakama lango la Heroes na katika dakika ya 86 ilifanya shambulizi baada ya Kibu Denis kuambaa na mpira kwa kasi kwenye lango la Heroes kabla ya kupiga krosi ya kimo cha mbuzi na kumkuta Msuva ambaye aliunganisha kwa kichwa lakini kipa wa Heroes, Yakoub Suleiman alikuwa macho.
Matokeo ya sare ya bila kufungana yanamaanisha kuwa ahadi ya Sh 10 milioni iliyotolewa kwa mshindi haikupata mwenyewe lakini pia ahadi ya Sh milioni moja kwa bao la kwanza ambalo lingefungwa katika uwanja huo nayo haikupata mwenyewe.
Uwanja wa Amaan ambao ni kati ya viwanja vikongwe vya soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, baada ya maboresho yaliyouweka katika hali ya ubora zaidi sasa utaitwa Amaan Complex ukiwa na maeneo ya kutumiwa kwa ajili ya michezo mingine mbali na soka.
Soka Kili Stars, Zanzibar Heroes hakuna mbabe
Kili Stars, Zanzibar Heroes hakuna mbabe
Read also