Na mwandishi wetu
Beki wa kulia wa Simba, Israel Mwenda (pichani) amesema ujio wa kocha Abdelhak Benchikha umemfanya ajihisi amezaliwa upya kutokana na kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Kabla ya Benchikha makocha waliopita Simba miaka ya karibuni; Pablo Franco, Zoran Maki, Juma Mgunda na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wote hawakumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Beki huyo alisema kwa muda mfupi ambao timu imekuwa chini ya Benchikha ameshacheza zaidi ya mechi nne na kutoa mchango mkubwa kwa timu yake hadi kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa.
“Nilikuwa najiona kama mtumishi hewa, nalipwa mshahara bila kufanya kazi lakini kwa sasa nafurahi kuwepo hapa, ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaipigania nembo ya Simba kufikia malengo yake msimu huu,” alisema Mwenda.
Beki huyo alisema habezi uwezo wa mtangulizi wake, lakini makocha waliopita hawakuwa na utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi wachezaji wengine kutoa mchango wao kwa timu zaidi ya kutumia baadhi ya wachezaji ambao anaamini ni msaada kwake.
Alisema kuna wakati hiyo ilimkatisha tamaa na kutamani kuvunja mkataba ingawa baadhi ya watu walimshauri kurudi kundini kuendelea kupigania nafasi ya kucheza.
Mwenda alijiunga na Simba misimu mitatu iliyopita akitokea KMC, lakini alikutana na upinzani mkali kutoka kwa Shomari Kapombe ambaye amekuwa chaguo la kwanza kwa makocha wengi wanaoifundisha timu hiyo.