Na mwandishi wetu
Timu ya Coastal Union imeachana na nyota wake watatu katika dirisha hili la usajili baada ya kushindwa kulishawishi benchi la ufundi chini ya kocha mkuu wa timu hiyo, David Ouma (pichani).
Wachezaji hao waliooneshwa mlango wa kutokea na Wagosi wa Kaya ni Fran Golubic, Juma Mahadhi na Mapinduzi Balama.
Akizungumza na GreenSports, Ofisa Habari wa Coastal, Abbas Elsabri alisema kuwa wanataka kutumia dirisha dogo la usajili kupunguza wachezaji walioshindwa kuwa kwenye mipango ya kocha mkuu.
“Tumeachana na wachezaji hawa kwa makubaliano ya pande mbili na yenye maslahi kwa kila mmoja tunawatakia kila la heri kwenye majukumu yao huko waendako, tunaheshimu mchango wao walipokuwa na sisi.
“Malengo yetu ni kuwa na kikosi chenye ushindani ambacho kitaenda kutimiza malengo yetu ya msimu hivyo lazima tuwe imara kwani ligi imekuwa ngumu kwa kila timu kupambana kupata matokeo,” alisema Elsabri.
Alisema kuwa wanatarajia kuongeza nyota wanne wapya kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao na mambo yakiwa tayari watawaweka wazi wachezaji wao wapya.