Na mwandishi wetu
Simba imepata pigo katika Ligi Kuu NBC baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na KMC wakati mahasimu wao Yanga wakitoka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Tabora United.
Katika mechi hizo zilizochezwa Jumamosi hii, Simba ikiwa Azam Complex, ilishitushwa na KMC dakika ya 31 baada ya Waziri Junior kufunga bao na kuifanya KMC iende mapumziko ikiwa mbele.
Juhudi za Simba zilizaa matunda katika dakika ya 57 baada ya kupata bao la kusawazisha lililowekwa kimiani na Saido Ntibazonkiza kwa mkwaju wa penalti.
Dakika mbili baadaye Simba waliongeza bao la pili lililowekwa kimiani kwa kichwa na Jean Baleke baada ya kuinasa krosi ya Shomary Kapombe.
Matarajio ya Simba kutoka uwanjani na pointi zote tatu yalizimwa katika dakika ya 89 baada ya Waziri Junior kuipatia KMC bao la pili akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Tepsi Evans.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kubaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 23 katika mechi 10 wakati KMC imefikisha pointi 17 ikiwa katika nafasi ya saba.
Kwa upande wa Yanga iliyokuwa ugenini mjini Dodoma kwenye dimba la Jamhuri, ilinufaika na bao pekee la Aziz Ki na kutoka na ushindi ambao umeiimarisha timu hiyo katika nafasi ya pili ya ligi hiyo.
Yanga sasa imekusanya pointi 30 tofauti ya pointi moja mbele ya Azam inayoshika usukani wa ligi hiyo wakati Tabora inabaki nafasi ya 12 na pointi zake 15.
Ligi hiyo kwa sasa imesimama kupisha mashindano ya kila mwaka ya Kombe la Mapinduzi pamoja na maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2024) zitakaofanyika mwakani nchini Ivory Coast.
Soka Yanga yatamba, Simba yakwama
Yanga yatamba, Simba yakwama
Read also