Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya (pichani) amesema atapambana kuhakikisha mpira unachezwa kila kona ndani ya mkoa huo.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa DRFA uliofanyika Jumamosi hii, Nyambaya alisema katika kufanikisha hayo wana mikakati kabambe kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa kitovu cha soka,
Alisema kuwa mpango wao ni kuhakikisha wanazalisha wachezaji lakini pia wanaimarisha miundombinu mbalimbali itakayorahisisha malengo yao kutimia.
“Niwapongeze wenyeviti wangu wa vyama vya wilaya kwa kazi nzuri wanayoifanya, ukweli Dar es Salaam tunaongoza kwa kuzalisha vipaji katika timu zote zinazoshiriki ligi mbalimbali zinazotambulika na TFF niwaambie pamoja na hilo bado tuna kazi ya kufanya kuhakikisha mpira unachezwa kila kona.
“Lengo la DRFA kwa mwaka ujao ni kuweka mazingira rafiki ili kushawishi vijana kucheza mpira na kuanzisha mashindano mengi ambayo yatasaidia kuibua vipaji vitakavyokuja kuwa tegemeo kwa taifa la Tanzania siku zijazo,” alisema Nyambaya.
Naye Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, Almas Kasongo alimpongeza Nyambaya kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuuinua mpira wa Dar es Salaam akisema ni kiongozi wa mfano kutokana na uongozi wake kutokuwepo na lawama kutoka upande wowote.
Kasongo alisema pamoja na mazuri hayo lakini amemtaka kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza soka la vijana, kutoa kozi za makocha, madaktari wa michezo na waamuzi na kusimamia vyema soka la wanawake na mafunzo ya utawala sababu hizo ndio shughuli za msingi za mchezo wa soka.
“Mafunzo ni kitu muhimu sana katika mustakabali wa chama kukuwa, kwa hiyo Nyambaya kazi unayoifanya inaonekana lakini usiridhike na mafanikio haya endelea kupambana ili mpira uchezwe zaidi ya ilivyo sasa,” alisema Kasongo.
Soka DRFA yataka soka lichezwe kila kona Dar
DRFA yataka soka lichezwe kila kona Dar
Related posts
Read also