Luxembourg City, Luxembourg
Mahakama ya Haki Ulaya (ECJ) imebariki kuanzishwa kwa Supa Ligi ya Ulaya (ESL) licha ya klabu kubwa kuikataa ligi hiyo huku rais wa Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin akisema ‘anaisubiri’ ligi hiyo ya timu mbili.
Uamuzi wa mahakama hiyo ulifikiwa jana Alhamisi kwa hoja kwamba ni kinyume cha sheria kwa Uefa kuzizuia klabu kujiunga na ESL, ligi ambayo inaaminika kuwa itatoa upinzani kwa ligi za soka za Uefa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Ceferin (pichani juu) alisema kwamba hawatohangaika kuwazuia badala yake anayasubiri mashindano ya timu mbili.
“Hatutojaribu kuwazuia, wanaweza kuanzisha wanachotaka wao, soka si kwa ajili ya biashara” alisema Caferin.
Mpango wa kuanzishwwa kwa ESL ambao unasimamiwa na kikundi cha A22 ambao ulianza kupata nguvu mwaka 2021, unataka kuwa na ligi itakayojumuisha timu kutoka klabu 64 za wanaume na 32 za wanawake.
Klabu za soka barani Ulaya zilikuwa za kwanza kuupinga mpango wa A22 zikiwamo zile za Ligi Kuu England (EPL) ambapo taarifa ya EPL ilieleza kuwa wataendelea kuupinga mpango wa ESL.
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Man City wamesisitiza msimamo wao wa kutoshiriki ESL kwa hoja kwamba wanaendelea kushiriki katika taratibu na misingi ya soka la Ulaya.
Man United, Chelsea na Tottenham Hotspur nazo pia zimeahidi kuendelea kushiriki michuano ya Uefa wakati Bayern Munich nayo imeweka wazi msimamo wake wa kuendelea kufunga milango ya mpango wowote wa ESL.
Man City, Chelsea, na Spurs ni kati ya timu sita zilizohusika katika mpango wa awali wa kuanzishwa kwa ESL lakini kwa sasa zimeukataa mpango huo baada ya kupigwa vita kila kona.
Akizungumzia uamuzi wa ECJ, Ceferin alisema kwao ni fursa ya kuboresha baadhi ya kanuni za Uefa baada ya kujikuta wakilaumiwa kwa mfumo wanaoutumia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, na kanuni hizo mpya wanatarajia zitaanza kutumika katika msimu wa 2024-25.
Naye Rais wa Umoja wa Klabu Ulaya (ECA), Nasser Al-Khelaifi kutoka klabu ya PSG ya Ufaransa alisema kwa wakati huu klabu zinayatambua mashindano bora duniani ni yale ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Hatutaki kumtisha au kumzuia yeyote, fanyeni mashindano yenu, ni sawa lakini mashindano bora ya klabu duniani ni Ligi ya Mabingwa, ni ‘chata’ ambayo imekuwapo miaka na miaka,” alisema Al- Khelaifi.
Mpango wa ESL ulianza rasmi Aprili 2021 kwa timu 12 zikiwamo za EPL, Chelsea, Arsenal, Man United, Liverpool, Man City na Spurs ambazo zilisaini makubaliano ya kushiriki ligi hiyo mpya.
Kati ya klabu hizo 12 hadi sasa zimebaki mbili tu za Real Madrid na Barcelona ambazo zimeshikilia msimamo wa kuanzishwa kwa ligi hiyo mpya ya soka barani Ulaya.
“Natumaini wataanzisha mashindano yao haraka iwezekanavyo wakiwa na timu mbili, niliangalia kilichoitwa andiko la A22, ni ngumu kuamua kama utakuwa na mshtuko au kukerwa na ‘onyesho’ lenyewe ambalo tayari limepingwa na kila mtu,” alisema Caferin.