Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amesema ataendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wanaojituma siyo kwa kuangalia jina wala umaarufu wao.
Benchikha pia amemtaka kila mchezaji kutimiza wajibu wake ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa katika mashindano yote wanayoshiriki.
Kocha huyo raia wa Algeria alisema yeye ni kocha mwenye kusimamia misingi na kuamini kile kinachofanywa na mchezaji uwanjani bila kujali kama watachelewa kupata mafanikio.
“Nitaendelea kusimamia kauli yangu ya kutoangalia jina la mchezaji, ninachotaka kwenye kikosi changu ni kila mchezaji awajibike kutimiza malengo ya timu, Simba ni timu kubwa na kila mchezaji ana uwezo ndiyo maana yupo hapa lakini kusajiliwa Simba siyo kutimiza malengo, kinachotakiwa ni uwajibikaji ndani ya uwanja,” alisema Benchikha.
Alisema kwa siku chache ambazo amekaa na timu hiyo amebaini uwezo mkubwa wa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa hawatumiki lakini chini ya utawala wake atahakikisha anawajengea ari na kujiamini ili kuwatumia katika mechi zijazo za mashindano yote.
Alisema alianza kufanya hivyo kwenye mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC ambapo aliwapa nafasi wachezaji watatu ambao tangu wasajiliwe hawajacheza hata mchezo mmoja.
Benchikha amewaomba viongozi na mashabiki kumpa ushirikiano katika mpango wake ambao lengo ni kutengeneza timu bora isiyotegemea uwepo wa mchezaji mmoja au wawili pekee.