Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Mashujaa FC, umefufua matumaini ya kuendelea kupata ushindi katika mechi zijazo za Ligi Kuu NBC.
Kocha huyo alisema lengo lao kubwa kwa sasa ni kujinasua katika nafasi ya mwisho waliyopo baada ya mfululizo wa matokeo mabaya waliyoyapata kwenye mechi zilizopita.
“Nawapongeza wachezaji wangu walicheza kwa kujituma muda wote wa mchezo, ni wazi hata wao wenyewe hawafurahishwi na matokeo tunayoyapata, naamini ushindi huu utakuwa chachu ya kuendelea kufanya vizuri mechi zijazo na kuondoka kwenye nafasi tuliyopo,” alisema Katwila.
Katwila alisema kuhakikisha wanaendeleza ushindi wamepanga kusaijili wachezaji wenye uzoefu wasiopungua watatu hadi wanne kwenye dirisha dogo ili kuimarisha sehemu zenye mapungufu.
Alisema pamoja na mwenendo wa kusuasua lakini anafurahi kuona timu yake inacheza soka la kuvutia ispokuwa kinachokosekana ni ushindi na tayari ameanza kulifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi.
Mtibwa Sugar pamoja na ushindi huo imeendelea kubaki nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi, ikifikisha pointi nane ikiwa imeshinda mechi mbili, sare mbili huku ikipoteza michezo 10.