Na mwandishi wetu
Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Morocco amesema kilichomuondoa katika kikosi cha Geita Gold ni majukumu ya kwenye timu ya taifa kuelekea michuano ya Afcon 2023.
Morocco alisema kwamba ameshatoa taarifa rasmi ya barua kwa uongozi wa Geita Gold na tayari wamempa ruhusa ya kuendelea na majumu yake kwenye timu ya taifa kama alivyotaka kupitia barua yake.
“Nimeuandikia barua uongozi nikitaka kukaa pembeni kutokana na majukumu ya timu ya taifa sababu Afcon inaanza muda si mrefu na nitakuwa na timu kwa takribani miezi miwili ndio maana nikaamua kuwaeleza kilichopo na wamenikubalia,” alisema Morocco.
Akifafanua zaidi, Morocco alisema kwamba kwa mujibu wa mkataba wake na Geita, haikuwa ngumu kwake kuondoka katika timu hiyo kwa kuwa suala hilo lipo wazi.
Alisema kwamba kwa sasa tayari yupo kwenye majukumu ya Taifa Stars na wanaendelea na utaratibu wa kuchagua wachezaji ambao watakwenda kwenye michuano ya Afcon ambayo itaanza kutimua vumbi Januari 13 hadi Februari 11, mwakani nchini Ivory Coast.
Morocco amekuwa na Geita Gold tangu mwanzoni mwa msimu huu na ameiongoza katika mechi 12 na kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na rekodi ya ushindi wa mechi tatu, sare nne na kufungwa mechi tano.
Katika mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu NBC akiwa na Geita, Morocco aliishuhudia timu hiyo ikikutana na kichapo cha mabao 3-1 mbele ya Coastal Union.
Baada ya kuondoka kwa Morocco, zipo habari kwamba Geita imekuwa katika mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Namungo, Denis Kitambi ili ainoe timu hiyo.
Soka Stars yamtoa Morocco Geita Gold
Stars yamtoa Morocco Geita Gold
Read also