Na mwandishi wetu
Uchezaji wa timu ya Simba chini ya kocha Abdelhak Benchika, umemfurahisha mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Ismail Rage akiamini kwa mwendo huo lazima waizamishe Wydad AC katika mechi yao ya Jumanne ijayo.
Rage ameeleza kufurahishwa na mabadiliko ya timu hiyo kwa sasa baada ya mechi tatu alizoongoza Benchikha tangu atue wiki mbili zilizopita, ikiwemo ya ushindi wa mabao 3-0 majuzi dhidi ya Kagera Sugar.
“Timu inacheza vizuri kwa kweli na hiki ndicho wanachotaka wanachama na mashabiki, inatupa nguvu kwa sasa na hata hiyo siku ya Jumanne tutajitokeza kwa wingi kujaza uwanja ili tuwafunge Wydad, yaani ni lazima Wydad ‘afe’ hapa.
“Matumaini yamerudi na wanaonekana wachezaji wenyewe wana ari, wana nguvu, wanahangaika, wanataka matokeo, Wydad lazima tumfunge na bahati nzuri tunacheza saa 10 jioni na kwa hali ya hewa ya muda huo itawashinda na itatupa faida sisi,” alisema Rage.
Rage ambaye pia amewahi kuwa katibu mkuu wa FAT sasa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), alishauri kusajiliwa washambuliaji wawili ili kuongeza ufanisi kwenye ufungaji kwani eneo hilo pekee kwa sasa ndilo linaonekana kushindwa kumalizia kazi nzuri inayofanywa na timu nzima.
Benchikha ameiongoza Simba katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa, akipata sare ya 0-0 dhidi ya Jwaneng na kupoteza 1-0 dhidi ya Wydad akiwa ugenini kabla ya kuifumua Kagera na Jumanne atawaongoza Wekundu hao dhidi ya Wydad kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam wakipambania ushindi wa kwanza wa michuano hiyo.