Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu ameeleza kuwa hana la kufanya kwa wanaomkosoa na kumpigia kelele katika uongozi wake kwani anaendelea na ujenzi wa timu hiyo kufanya vizuri.
Mangungu ameeleza hayo baada ya kuibuka hoja kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakimtaka ajiuzulu kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo hasa baada ya kufungwa mabao 5-1 na Yanga Novemba 5, mwaka huu.
Kiongozi huyo alisema kwake anaona ni kawaida kukosolewa kibinadamu kwani haiwezekani akakubalika na watu wote na zaidi wanaofanya hivyo wanatumia haki yao ya msingi hivyo ni suala ambalo linaeleweka kibinadamu na lipo siku zote.
“Ni kawaida kwa maisha ya biandamu, huwezi ukakubalika, ukapokelewa na watu wote na huwezi ukakataliwa au ukakosolewa na watu wote.
“Wanaokosoa wanatumia haki yao, mara nyingine mtu akikosoa anapata furaha, basi kama ni jambo linalompa furaha aendelee kukosoa lakini kimsingi tunaendelea kuhakikisha tunajenga mazingira mazuri ya timu yetu kufanya vizuri,” alisema Mangungu.
Kuhusu mwenendo wa Simba kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi dhidi ya Wydad AC, Mangungu alisema hana wasiwasi na timu hiyo kwani ina uzoefu wa kutosha na magumu ya michuano hiyo, hivyo anaamini itakaa sawa na watapata mafanikio muda si mrefu.
Katika hatua ya makundi msimu huu, Simba imetoa sare mechi mbili na kufungwa moja na hivyo kuburuza mkia kwenye Kundi B ikiwa na pointi mbili. ASEC Mimosas inaongoza kwa pointi saba, ikifuatiwa na Jwaneng Galaxy yenye nne na Wydad AC yenye pointi tatu.