London, England
Beki wa Man United, Harry Maguire na kocha wake Erik ten Hag wameshinda tuzo za mchezaji na kocha bora kwa mwezi Novemba, tuzo ambayo ina maana kubwa zaidi kwa Maguire aliyepitia kipindi kigumu.
Man United imepoteza mechi nne kati ya saba za mwanzo za Ligi Kuu England (EPL) kabla ya kujitutumua na kupaa hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Katika kipindi cha mwezi Novemba timu hiyo imeshinda mechi zake dhidi ya Fulham, Luton na Everton, mechi ambazo Maguire alicheza zote baada ya kupitia kipindi kirefu cha kusugua benchi kilichoandamana na lawama za kufanya makosa ya kizembe pale alipopata nafasi ya kucheza.
Kwa kushinda tuzo hiyo, Maguire anakuwa beki wa kwanza kufanya hivyo tangu Januari 2009 baada ya beki mwingine wa timu hiyo, Nemanja Vidic naye kushinda tuzo hiyo.
Hadi kuibuka kinara wa tuzo hiyo, Maguire aliwabwaga Anthony Gordon wa Newcastle, Jeremy Doku wa Man City, Raheem Sterling wa Chelsea, Marcus Tavenier wa Bournemouth na kipa wa Luton, Thomas Kaminski.
“Nisengeweza kushinda bila ya wachezaji wenzangu, maofisa wa timu na mashabiki, mapenzi yenu na sapoti vyote haviwezi kupita hivi hivi, nashukuru,” alisema Maguire.
Wakati akiwa katika kipindi kigumu Man United, Maguire alivuliwa unahodha na Ten Hag mwezi Julai na mipango ikaanza ya kumpiga bei lakini aliikataa ofa ya West Ham na kuamua kubaki United licha ya kusugua benchi.