Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema hatma ya winga wa timu hiyo Jadon Sancho kurudi katika kikosi cha kwanza ipo mikononi mwa mchezaji huyo mwenyewe.
Sancho, 23 amekuwa akifanya mazoezi ya peke yake mbali na kikosi cha kwanza baada ya kuwapo madai kwamba ‘alitolewa kafara’ kwa kuachwa katika mechi dhidi ya Arsenal mwezi Septemba.
Ten Hag alisema kwamba alimuweka kando Sancho kwa sababu kiwango chake mazoezini kilikuwa chini jambo ambalo mchezaji huyo hakukubaliana nalo na kudai kuwa kocha ni kama alimtoa kafara.
“Anajua anachotakiwa kufanya, ni yeye mwenyewe kuamua,” alisema Ten Hag kuhusu hatma ya winga huyo aliyesajiliwa mwaka 2021 kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 73 milioni.
Ten Hag amekusudia kuimarisha nidhamu katika timu hiyo jambo ambalo amekuwa akilifanyia kazi tangu ajiunge na timu hiyo takriban miezi 18 iliyopita.
Kauli ya kocha huyo ilikuja baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari kuhusu hatma ya Sancho na habari ya kuuzwa katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani.
“Kitakachotokea huko anakijua na anajua nini anatakiwa kufanya, kama anataka kurudi (kikosi cha kwanza) ni uamuzi wake,” alisema Ten Hag.
“Ni suala la taratibu na kila mchezaji ni lazima awe katika viwango fulani na suala lililojitokeza ni hilo,” alisema Ten Hag.