Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema hajashangazwa na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kwani hiyo inatokana na ubora wa timu waliyonayo kwa sasa.
Dabo alisema mtihani walionao sasa ni kuendelea kujipanga zaidi dhidi ya wapinzani wanaofuata kwa sababu watakuja kwa tahadhari kutokana na vipigo wanavyovitoa kwa sasa kwa kuwa hata mechi yao iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar walishinda mabao 5-0 pia.
“Si kazi rahisi kupata ushindi wa hivi bila kuruhusu bao lakini haijatushangaza sababu tuna ari na ubora wa kufunga mabao mengi, na sasa tunahitaji kuendelea kukaa vizuri zaidi wapinzani watakaoukuja watajaribu kuzuia hicho kitu, hivyo tutazidi kujiweka sawa katika hilo,” alisema Dabo.
Kocha wa KMC, Abdihamid Moallin alisema kilichotokea mpaka kupoteza mchezo huo kwa bao nyingi ni kubaki kwenye mtindo wao wa kucheza soka na kuwashambulia wapinzani, lakini kama wangebadili mipango yasingewakuta hayo ingawa wanachukulia kupoteza huko ni kama funzo kwao.
“Wakati mwingine unapobaki kwenye mipango yako ndicho kinachotokea unapocheza na timu nzuri kama Azam lakini kupoteza huku tumechukua kama funzo kwetu kwa ajili ya kuendelea kuimarika maana tuna timu nzuri ya vijana wapambanaji hivyo hili ni somo kwetu na tutakwenda kujiweka sawa zaidi,” alisema Moallin.
Kwa matokeo hayo Azam imetoka nafasi ya pili na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi 25 baada ya mechi 11 huku KMC ikiendelea kusalia kwenye nafasi ya tano kwa pointi 19 baada ya mechi 12.