Madrid, Hispania
Klabu ya Real Madrid ya Hispania inadaiwa ipo tayari kumsajili mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe kama tu mchezaji huyo atakubali na wameweka hadi Januari 15 mwakani awe amefikia uamuzi.
Uamuzi wa Real Madrid huenda ukaibua vita baina ya timu hiyo na Liverpool ambao hivi karibuni wameonesha nia ya kumtaka mshambuliaji huyo iwapo mshambuliaji wao tishio, Mohamed Salah atatimkia Arabuni.
Mbappe anadaiwa kutaka changamoto mpya nje ya PSG lakini ni vigumu kufahamu kama atakubaliana na sharti la Real Madrid, klabu ambayo ilitaka kumsajili msimu uliopita lakini ikashindikana.
Kuhusu Liverpool, hivi karibuni habari ya Salah kutakiwa Saudi Arabia imezidi kupata nguvu hali iliyowafanya mabosi wa timu hiyo kuanza hesabu za kuziba pengo ikitokea akaondoka na Mbappe anaonekana kuwa mtu sahihi kuziba pengo hilo.
Mkataba wa Mbappe na PSG unafikia ukomo Juni mwakani na kabla ya kuanza kwa msimu huu, mchezaji huyo aliingia katika mzozo na mabosi wa PSG waliomtaka asaini mkataba mpya au auzwe.
Mzozo huo ulimalizwa ingawa haikuweza kufahamika nini hasa walichokubaliana na kwa hali hiyo haitoshangaza kumuona akiendelea kuichezea PSG kwa kusaini mkataba mwingine.
Kwa upande mwingine, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti anaonekana kutosumbuliwa sana na Mbappe licha ya ubora wa mshambuliaji huyo na kuna wakati aliwahi kunukuliwa akisema kwamba timu yake ipo sawa bila ya huduma ya Mbappe.
Kimataifa Real yamgeukia Mbappe kwa masharti
Real yamgeukia Mbappe kwa masharti
Read also